Muziki
Chino Kid aingia anga za Mudara

MAREKANI:STAA wa Bongo Fleva, Chino Kid, anatarajiwa kuendelea kutamba kwenye muziki kupitia kolabo yake mpya na Mudara, ambayo inatarajiwa kutoka hivi karibuni.
Mudara ni miongoni mwa wasanii wapya wanaokuja kwa kasi kwenye muziki wa Bongo Fleva, akitokea Marekani ambako anaishi kwa sasa. Kwa sasa, anafanya vizuri na wimbo wake Osiyaa, ambao umemfungulia milango kwenye vyombo vikubwa vya habari hapa nchini.
Akizungumza na Spoti Leo, Mudara (jina kamili Ally Mudara) amesema kuwa kolabo yake na Chino Kid itamfungulia fursa zaidi kwenye sanaa yake, ambayo anaipigania akiwa ughaibuni.
“Muda wowote kuanzia sasa, nitatoa kolabo hii niliyofanya na Chino Kid. Inajulikana wazi kuwa Chino Kid hana kazi mbovu, na mimi pia nimeonyesha uwezo wangu mwingine kwenye hii ngoma. Ikitoka, itanipa mashabiki wengi zaidi hasa Afrika Mashariki,” amesema Mudara.
Ameongeza kuwa mafanikio ya ngoma yake Osiyaa yamempa nguvu ya kuwekeza zaidi kwenye kazi zake, ikiwemo kolabo na Chino Kid ambayo anaamini itampaisha zaidi kwenye tasnia ya muziki.
“Itaniongezea namba kwenye platforms zote za muziki, mashabiki wataweza kupakua na kusikiliza ngoma hiyo pamoja na nyingine nyingi nitakazoziachia baadaye. Lengo kubwa la hii kolabo ni kutanua wigo wangu wa kusikika kwenye mitandao,” ameongeza.
Aidha, Mudara ameweka wazi kuwa ana mpango wa kuendelea kushirikiana na wasanii wa Tanzania licha ya kuishi Marekani, kutokana na mapokezi mazuri na upendo mkubwa kutoka kwa mashabiki wa Afrika Mashariki.
Akizungumzia maendeleo ya muziki wa Bongo Fleva, Mudara amesema anafurahia kuona mastaa wakubwa kama Diamond Platnumz, Alikiba, Jux, Rayvanny, Harmonize, Abby Chams na wengine wakiendelea kufanya vizuri na kuipeperusha vema bendera ya Tanzania kimataifa, huku wakipewa sapoti ya karibu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.




