Barca yamuweka chini Flick

BARCELONA:UONGOZI wa Klabu ya FC Barcelona unapanga kumuongeza mkataba kocha mkuu wa kikosi hicho Hansi Flick, mkataba utakaomuweka kwenye viunga vya Camp Nou hadi 2027 na inapangwa kusainiwa rasmi mapema mwezi Mei.
Taarifa kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika ndani ya klabu ya Barcelona vimenukuliwa na vyombo vya habari nchini Spain kuwa uongozi wa klabu hiyo unaridhishwa na mwenendo wa Flick ambaye ameiwezesha klabu hiyo kukaa kileleni mwa Laliga na nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Flick na Barcelona wamekuwa na majadiliano tangu mwezi Februari mwaka huu na sasa kuna mwanga wa kocha huyo kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja zaidi kwenye mkataba wake wa sasa unaotamatika 2026.
Taarifa zinaeleza zaidi kuwa awali kulikuwa na mvutano baina ya pande hizo mbili wakati uongozi wa Barcelona ukitaka kumuongeza Flick miaka miwili wakati kocha huyo akipendelea kuongeza mkataba kwa mwaka mmoja mmoja sharti ambalo uongozi umekubaliana nae.