Diamond Platnumz kufanya onesho kubwa Uingereza

DAR ES SALAAM: MSANII maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Nassib Abdul, maarufu kama Diamond Platnumz, anatarajiwa kufanya onesho kubwa nchini Uingereza tarehe 13 Juni mwaka huu, katika ukumbi maarufu wa Royal Albert Hall, uliopo jijini London.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Diamond aliandika: “Watu wangu wapendwa, nataka tu kuwakumbusha kwamba kijana wenu mnyenyekevu na mwenye heshima atakuwa akitumbuiza mubashara kwenye ukumbi wa Royal Albert, Uingereza, Juni 13.”
Msanii huyo amesema kuwa ataandaa onesho la kuvutia lenye mambo ya kushangaza, ambapo atatumbuiza nyimbo zake mbalimbali zinazopendwa na mashabiki kutoka mataifa tofauti duniani.
Onesho hilo ni sehemu ya mkataba mkubwa wa kimataifa aliotia saini na kampuni ya Showtime Promotions kwa kushirikiana na Baron Inc, ambao unatarajiwa kumpeleka kwenye ziara ya kimuziki katika miji 10 mikubwa barani Ulaya na Amerika.
Kwa sasa, Diamond anatikisa anga ya muziki na wimbo wake mpya uitwao “Kuna”, huku ratiba rasmi ya ziara hiyo bado haijawekwa wazi.




