Nyumbani

Watanzania waaswa kulinda utamaduni

DAR ES SALAAM: WATANZANIA wametakiwa kulinda utamaduni na kudumisha maadili ya Kitanzania, ikiwa ni pamoja na kuwa mabalozi wa lugha ya Kiswahili katika ngazi zote za kijamii na kimataifa.

Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati wa uzinduzi wa mfumo wa AMIS kusaidia kujisajili na kanzi data wasanii katika kufanya kazi zao, sambamba na kikao kazi cha 15 cha Maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri mbalimbali nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanawapa Maafisa Utamaduni nafasi ya kufanya kazi zao ipasavyo, kwa lengo la kudumisha maadili na tamaduni za Kitanzania.

“Wakurugenzi wa Halmashauri wapeni nafasi Maafisa wa Utamaduni waweze kudumisha maadili kwa kuhamasisha wananchi,” amesema Majaliwa.

Kuhusu lugha ya Kiswahili, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wake katika kuiwakilisha Tanzania kimataifa na kuitangaza vyema katika mataifa mengine.

“Lugha ya Kiswahili ni pana, na kwa hakika inalitangaza Taifa letu huko nje. Hata mabalozi wetu tunawasisitiza kufungua shule za Kiswahili katika maeneo wanakowakilisha nchi yetu,” ameongeza.

Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Mwita Maulid, alisisitiza umuhimu wa kudumisha Muungano kwa njia ya kulinda na kuenzi utamaduni wa pande zote mbili za Muungano.

“Nikuhakikishieni kuwa sisi kama Wizara tutaendelea kudumisha Muungano wetu kwa kulinda maadili na utamaduni wa Tanzania,” alisema Tabia Mwita.

Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa Tanzania Bara, Profesa Paramagamba Kabudi, alieleza kuwa Tanzania ni mfano wa kuigwa barani Afrika kwa mshikamano wa makabila na utunzaji wa mila.

“Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika yenye wingi wa makabila lakini yenye mshikamano na umoja wa kipekee. Ni muhimu kulinda utamaduni wetu,” amesema Prof. Kabudi.

Related Articles

Back to top button