Muziki

Jembe ni Jembe na Steve Nyerere wakabidhi viti vya walemavu Mtoko wa Pasaka

DAR ES SALAAM:MENEJA wa msanii Harmonize, Sebastian Ndege maarufu kama Jembe ni Jembe, kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere, wamekabidhi viti vya magurudumu kwa watu wenye ulemavu katika tamasha la Mtoko wa Pasaka lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Steve Nyerere alimshukuru Jembe ni Jembe kwa moyo wake wa huruma na kujitolea kwa ajili ya jamii.

“Nikushukuru ndugu yangu kwa kujitoa kwa dhati kuwasaidia watu wenye ulemavu. Kwa kuwapatia viti vya magurudumu, umeweza kugusa maisha ya Watanzania wenye uhitaji mkubwa. Umetoa faraja na matumaini kwao,” alisema kwa hisia.

Aliongeza kuwa awali alikuwa mzito kiroho, lakini kupitia huduma na ibada zilizofanyika kwenye Mtoko wa Pasaka, amejiona mwepesi na mwenye furaha ndani ya ibada za kusifu na kuabudu.

Kwa upande wake, Jembe ni Jembe alisema kuwa Mtoko wa Pasaka ni tamasha lenye kuwaleta pamoja Watanzania wapenda nyimbo za Injili, hivyo aliona ni nafasi sahihi ya kutoa faraja kwa watu wenye ulemavu ili nao wafurahie Sikukuu ya Ufufuko wa Kristo.

“Tamasha hili limekuwa chachu ya furaha kwa wengi. Nikaona si vyema kuja mikono mitupu, bali niwashirikishe faraja wale wanaohitaji zaidi. Ni furaha yangu kuona wakifurahia na kushiriki nasi ibada ya Pasaka,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi, akisisitiza umuhimu wa kutotamani machafuko kama yanayoshuhudiwa katika baadhi ya mataifa mengine.

“Tuilinde amani yetu, tuienzi na kuitunza. Amani ni zawadi kubwa ambayo inafanya Taifa letu kuwa la kupendwa na watu wengi,” aliongeza.

Mtoko wa Pasaka umeendelea kuwa jukwaa la ibada, burudani, na huduma kwa jamii, ukiwakutanisha waimbaji, viongozi wa dini, wasanii wa fani mbalimbali, na watu maarufu kutoka kona zote za nchi.

Related Articles

Back to top button