
KOCHA Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema klabu yake inakabiliwa na michezo migumu inayofuata hivyo ni lazima kuhakikisha inajiandaa kushinda mechi hizo.
Katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara Yanga ikiwa mwenyeji ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya watani wake wa jadi Simba.
Akizungumza katika mkutano na waadishi wa habari Dar es Salaam leo kuelekea mchezo wa ligi dhidi ya KMC Oktoba 26 amesema kwa sasa sio suala la nani atacheza ila jambo muhimu ni kupata alama tatu.
“Tunafahamu kuwa ratiba yetu ni ngumu, tunafanya kila jitihada kuendana na uhalisia unaotukabili kwa sasa. Tuna mechi ngumu mbele yetu na huo ndio ukweli ambao tunapaswa kupambana nao,” amesema Nabi.
Yanga itacheza mwingine wa ligi Oktoba 29 dhidi ya Geita Gold kabla ya kuikabili Club Africain katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika Novemba 2, 2022.