Muziki

Rose Muhando atema moto Mtoko wa Pasaka

“Hakuna kama yeye”

DAR ES SALAAM:MWIMBAJI mahiri wa muziki wa Injili, Rose Muhando, ameonesha kwa mara nyingine kuwa bado ni malkia wa muziki huo nchini, baada ya kuteka hisia za mashabiki katika tamasha la Mtoko wa Pasaka lililofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye ukumbi wa The Super Dome, Dar es Salaam.

Rose, anayefahamika kwa sauti ya kipekee na uwepo wa kisanii jukwaani, aliwafanya mamia ya mashabiki kusimama kwa shangwe kubwa alipoperform wimbo wake maarufu Amina. Umati uliungana naye kuimba na kucheza kwa hisia kali, hali iliyoufanya ukumbi kutetemeka kwa nderemo na vifijo.

Kilichovutia zaidi ni hatua ya Rose kuvua viatu jukwaani ili acheze kwa uhuru zaidi, huku akiruka na kutawala jukwaa kwa nguvu na furaha akiwa na madansa wake. Ujio wake huo ulithibitisha kuwa bado ana mvuto mkubwa kwa mashabiki wa nyimbo za Injili.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tamasha hilo, Rose alisema:
“Tumefurahi sana kwa tamasha hili. Ni mahali ambapo tunakusanyika pamoja kama waimbaji. Nawashukuru mashabiki kwa moyo wao wa upendo na kwa kucheza pamoja nasi. Mungu awabariki sana,” alisema kwa furaha.

Mbali na Rose, wasanii wengine waliopamba jukwaa hilo ni pamoja na Bella Kombo, aliyeimba wimbo Mungu ni Mmoja akishirikiana na Evelyn Wanjiru kutoka Kenya. Pia walikuwepo Zabron Singers, Paul Clement, Solomon Mukubwa (Kenya), Harun Laston ‘Zoravo’, Ambwene Mwasongwe, Kwaya ya Neema, na Kwaya ya Makuburi.

Mwimbaji Christina Shusho naye aliwashangaza wengi alipoimba wimbo Aniongoze Popote kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye.

Tamasha hilo pia lilikutanisha watu maarufu kutoka sekta mbalimbali akiwemo Madam Ritha, Sofia Kessy, Yusuph Mlela, na Chuchu Hans, pamoja na waumini wa dini zote, likiwa na lengo la kuunganisha watu kupitia muziki wa Injili na kuadhimisha Pasaka kwa namna ya kipekee.

Related Articles

Back to top button