Ligi Kuu

Kocha Matano amuondoa kipa baada kichapo cha Yanga

BABATI: KOCHA Mkuu wa Fountain Gate FC, Robert Matano, ametangaza kuachana na kipa wake namba moja, John Noble, akimtuhumu kwa makosa ya makusudi yaliyochangia kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo ulipigwa Jumatatu, Aprili 21, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara, ambapo Fountain Gate FC walishindwa kuhimili makali ya Yanga licha ya kuonesha jitihada kipindi cha kwanza.

Matano alieleza kuwa Noble alihusika moja kwa moja na mabao mawili ya kipindi cha kwanza kwa kufanya maamuzi yasiyoeleweka, hali iliyompa wasiwasi juu ya dhamira ya mchezaji huyo uwanjani.

“Kilichofanywa na kipa wetu, kupeana waziwazi mabao… tumeimiliki Yanga kipindi cha kwanza, lakini aliyoyafanya nyanda wetu sielewi kabisa,” alisema Matano kwa masikitiko.

Kocha huyo mkongwe aliongeza kuwa makosa hayo yameigharimu timu sana, hasa kwa kuzingatia nafasi yao katika msimamo wa ligi. Amesisitiza kuwa haoni sababu ya kumtumia tena Noble katika michezo iliyo mbele yao.

“Noble amechangia sana kutuumiza. Sijui kwanini amefanya vile, nadhani yeye atakuwa na majibu sahihi. Sifikirii kumtumia katika kikosi changu,” aliongeza.

Kwa sasa, Fountain Gate FC wapo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 29, na wanasalia na JKT Tanzania, Coastal Union na Azam FC.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button