Pacome kuikosa Fountain Gate

DAR ES SALAAM: KIUNGO Mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, hatakuwepo sehemu ya kikosi cha timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate FC unaotarajiwa kuchezwa Aprili 21, mjini Babati, Manyara.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema Pacome atakuwa nje ya uwanja kwa siku 14 akiuguza jeraha la kifundo cha mguu alilolipata wakati wa mchezo uliopita dhidi ya Azam FC, baada ya kugongana na mchezaji Yahya Zayd.
Kamwe amesisitiza kuwa jeraha hilo limetokana na rafu ya makusudi kutoka kwa mchezaji wa Azam. Licha ya kutokuwepo kwenye kikosi cha mechi hiyo, Pacome atasafiri na timu kuelekea Manyara kama sehemu ya maandalizi ya baadaye.
“Pacome atakuwa nje kwa wiki mbili sawa na siku 14. Hatacheza dhidi ya Fountain Gate FC, lakini atakuwa sehemu ya msafara wetu. Baada ya mechi hiyo, tutaelekea Zanzibar kujiandaa na Kombe la Muungano,” amesema Kamwe.
Kamwe ameongeza kuwa wakati timu ikiwa Zanzibar, jopo la madaktari litamfanyia uchunguzi kuhakikisha kama anaweza kurejea kwa wakati kabla ya fainali ya Kombe la Muungano.
Kuhusu safari ya kuelekea Manyara, Kamwe amesema kuwa timu itaondoka Dar es Salaam siku ya Jumamosi, Aprili 19, kwa kutumia treni ya SGR hadi Dodoma, na kutoka hapo watasafiri kwa basi hadi Babati kwa ajili ya mchezo huo muhimu.