Azam FC: Tutaendeleza tulipoishia

MBEYA:KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Badr Idriss, amesema wamejipanga kuhakikisha wanaendeleza ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KenGold utakaochezwa leo.
Azam FC itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, majira ya saa 10:00 jioni.
Kocha Idriss amesema wanapaswa kurejea tena kwenye ligi wakiwa na ari nzuri na matarajio makubwa yatakayowapa matokeo mazuri.
“Unajua mchezo wetu wa mwisho wa ligi tulishinda, na tunapaswa kuendelea hivi hivi ili kuipatia timu yetu morali. Wachezaji wote wapo tayari na wana matumaini ya kupata ushindi,” amesema.
Ameongeza kuwa wameiandaa timu kwa kupata michezo mingi ya kirafiki, ambapo ilikuwa ni nafasi nzuri kwa wachezaji ambao hawapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
“Unajua wachezaji wetu wengine walienda kwenye timu zao za taifa, ndiyo maana tulipata muda mzuri wa kujiandaa. Tumekuwa na vipindi vya mazoezi asubuhi na mchana, tuko tayari kupambana,” amesema.
Azam FC inashika nafasi ya tatu kwa pointi 48, huku KenGold ikishika mkia kwa pointi 16.