Diamond afunguka mapenzi na Rita, ‘Zuchu amenisamehe’

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz amejikuta tena katikati ya utata wa tuhuma za kimapenzi baada ya anayedaiwa kuwa mpenzi wake, Rita Norbeth kuvujisha picha na video zao za faragha mtandaoni.
Rais huyo wa WCB amekuwa ‘akitrend’ baada ya kutoa picha ambazo hazijawahi kuonekana, jambo ambalo lilimfanya ajibu.
Katika taarifa yake, Diamond amekiri kuwa awali alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke husika lakini akafafanua kuwa uhusiano wao uliisha mwaka 2023. Alimshtumu mwanamke huyo kwa kujaribu kumchafua kwa kuvujisha maudhui yao na kudai pesa.
Aidha alieleza kuwa suala hilo tayari limesharipotiwa kwenye mamlaka husika na amewatoa hofu mashabiki wake kuwa mpenzi wake wa sasa Zuchu anaifahamu hali hiyo na amemsamehe.
“Nimeona video zikisambaa mtandaoni ambazo zinanihusisha. Hizi ni klipu za zamani za 2023, na niliachana na mwanamke huyo karibu miaka miwili iliyopita. Tayari nimeshamweleza mwenzangu kila kitu. Hata hivyo, mwanamke huyo sasa anatumia klipu hizo, pamoja na jumbe za uwongo, kunilaghai ili kujinufaisha kifedha. Suala hilo limeripotiwa kwa mamlaka, na hatua za kisheria zinachukuliwa,” Diamond amesema.
Mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Rita, amekanusha madai ya Diamond, akisisitiza kuwa yeye ndiye aliyemaliza uhusiano wao Novemba 2024.
Amesema kuwa aliondoka baada ya kugundua kuwa hakuwa makini kuhusu uhusiano wao. Kulingana naye, madai ya Diamond kuwa waliachana 2023 ni ya uongo, kwani huo ndio mwaka ambao Zuchu aligundua uchumba wao.
Rita pia alidai kuwa jumbe zinazozungumziwa ni ya kuomba kodi ya nyumba ambayo Diamond aliahidi kumpatia lakini hakumlipia. Zaidi ya hayo, alimshutumu kwa kukosa uaminifu kwake na wanawake wengine walipokuwa pamoja nchini Afrika Kusini.
Kashfa hiyo imezua hisia tofauti mitandaoni, huku wengi wakihoji iwapo uhusiano wa Diamond na Zuchu unaweza kuhimili utata huo.