BurudaniFilamu

DEEP WATER: Ni mapenzi na kifo!

BAADA ya kuishi kwa muda mrefu na kufanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike, wanandoa Vic na Melinda Van Allen wanajikuta katika migogoro ya mara kwa mara, na sasa mambo hayaendi sawa kwenye ndoa yao.

Melinda yupo tayari kabisa kuondoka na kumwacha mume, lakini mume anaona hii isije kuwa tabu na kupeana talaka, hivyo anaamua kumruhusu mkewe akatafute furaha nje ya ndoa.

Kama mke akihitaji vya kuhitaji basi achepuke akavipate nje ya ndoa ila aendelee kubaki kuwa mke wa mwamba huyu hata kama hawashiriki chochote ili mradi waendelee kumlea mtoto wao kama wanandoa.

Ni suala gumu kweli kweli kwa mume kufikia hatua hii lakini ndiyo hivyo tena, mume hana namna nyingine ya kufanya na hataki mtoto wao Trixie aishi maisha ya bila wazazi wote wawili, na pia hataki jamii ione kama wawili hao wameachana.

Na jambo kubwa zaidi ni kwamba mwamba huyu bado anampenda sana mkewe na hayupo tayari kumpoteza kirahisi rahisi, pia anaamini kwamba ipo siku mkewe atajirudi na wataishi vizuri kama zamani.

Na kingine pia hataki ku… ah, au ngoja tuendelee na simulizi… Sasa, wawili hawa wanatoka pamoja na huko nje wanajifanya bado wapo kwenye mapenzi motomoto lakini ukweli wa hali ya penzi lao ni wao tu wanaojua kuwa taa nyekundu ilishawaka kitambo, na mke anajihusisha na wanaume wengine huku mume akiruhusu hilo kwa kuwa hataki mkewe aondoke.

Watu wanaowazunguka hawajui nini hasa kinaendelea kwenye familia hii, mume na mke wanaendelea kuishi nyumba moja na wakati mwingine wanakaa kitanda kimoja, wakati mwingine pia wanapiga stori kana kwamba hakuna tatizo.

Wakati mwingine pia wanazungumza mambo ya kugusa hisia ingawa ukweli hisia za mahaba kati yao zilishahama kitambo huku mke akiendelea kuchepuka na mabwana wengine, na mume anaona ingawa anajitahidi kumezea.

Ni ukweli usiopingika, inahitaji roho ngumu sana kumwona mke wa ndoa akiwa na wanaume wengine. Hiki ni kitu ambacho kinamuumiza sana huyu mwamba kwa sababu bado anampenda sana mkewe ila mke hamhitaji mumewe! Dah!

Kwa kweli inaumiza sana. Kwa kuwa mume hataki mambo yawe makubwa hivyo amemruhusu mkewe afanye anachokitaka ili aokoe jahazi ila ndani yake roho inamuuma sana.

Kibaya zaidi mke haishii tu kutoka na mabwana huko nje bali anaanza kuwaleta hadi ndani ya nyumba na mume akiwa humo humo ndani akishuhudia kila kitu, na wakati mwingine mume analazimika kula nao huku akiwaona wakifanyiwa yale ambayo yeye alikuwa anafanyiwa na mkewe.Dah!

Kama ni ukatili basi huu ni ukatili uliopitiliza! Inaumiza kweli kweli! Na hali hii si ya mara moja tu kwa mke kufanya hivi mbele ya mumewe, inaendelea hadi mume anaonekana kama zoba fulani hivi mbele ya mkewe.

Ni kama vile mke ameamua kufanya hivi makusudi ili kumuumiza mumewe ambaye pamoja na kumezea lakini ukweli ni kwamba anamuumiza sana.

Sasa hii ni tisa, kumi kuna tatizo kubwa sana linatokea; kila mwanamume anayechepuka na huyu bibie siku chache baadaye hukutwa akiwa amekufa na chanzo cha kifo hicho hakijulikani.

Na si tu kwamba wanaume hawa wanakutwa wamekufa bali wameuawa kikatili na aliyehusika na mauaji hayo hajulikani! Polisi wanaingia kazini wakiwa mstari wa mbele katika kuchunguza mauaji hayo ili kufahamu ni nani aliye nyuma ya vifo hivyo.

Mke anaamini kuwa muuaji ni mumewe lakini mume anakataa kuhusika na vifo hivyo. Katika uchunguzi wao polisi wanashindwa kuthibitisha na wakati huo idadi ya vifo inazidi kuongezeka kwa kila mwanamume anayejaribu kumgusa mke wa mwamba! Dah, sasa hali inatisha sana badala ya kushtusha!

Hii ni filamu ya dakika 115 iliyotengenezwa nchini Marekani na Canada na kuachiwa hivi karibuni, mnamo Machi 18, 2022, ikiwa imetengenezwa kwa bajeti ya dola milioni 48.9.

Ili kuyajua yote itafute uitazame, hakika hautajutia muda wako, kwani kuna vimambomambo vitamu sana hasa kwa wanandoa, naamini wataielewa sana kazi hii kwani zile hisia za namna ambavyo mambo huendelea kwenye ulimwengu wa ndoa yatawagusa mno.

Ila wale ambao hawapo kwenye ulimwengu wa ndoa inaweza kuwa vigumu kuyaelewa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button