Muongozaji filamu India ajaribu kujiua

INDIA: MUONGOZAJI na muigizaji wa filamu nchini India, Sajid Khan, amesema aliwahi kujaribu kujiua mara kadhaa ndani ya miaka sita baada ya kukumbwa na tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kufukuzwa kazi.
Muongozaji huyo ambaye alikabiliwa na madai mengi wakati wa vuguvugu la ‘MeToo’ ndani ya Bollywood, ameweka wazi athari alizozipata wakati wa sakata hilo katika maisha yake ya kibinafsi na ya kikazi.
Amesema mnamo mwaka wa 2018, walipokuwa wakitengeneza filamu ya ‘Housefull 4’, wanawake kadhaa walimshutumu Khan kwa unyanyasaji wa kijinsia, tuhuma ambazo zilimsababisha akaondolewa katika mradi huo na pia alisimamishwa kazi.
Katika mahojiano ya wazi na Hindustan Times, Sajid amefichua kwamba baada ya tuhuma hizo alikumbwa na matatizo ya kiakili na kihisia ndani ya miaka sita iliyopita kiasi cha kutaka kukatisha uhai wake mara kadhaa.
“Nilifikiria kukatisha maisha yangu mara kadhaa katika miaka sita iliyopita, kutokana na kuzongwa na tuhuma hizo,” ameeleza Sajid.
Hata hivyo Sajid amesema Jumuiya ya Wakurugenzi wa Filamu na Televisheni ya India (IFTDA) kumuondoa katika kifungo hakuweza kupata nafasi kwenye tasnia ya filamu tena sababu aliyumba kiuchumi.
“Tangu umri wa miaka 14, nimekuwa nikipata pesa kwa ajili ya familia yangu, lakini baada ya tuhuma hizo nilikumbwa na jukumu zito baada ya kifo cha baba, ambaye alikuwa muongozaji na mtayarishaji wa filamu, Kamran Khan, lakini alifariki akiwa ameaacha madeni mengi hivyo nilipaswa kuyalipa nami sikuwa na fedha ikanilazimu niuze nyumba yangu na kuhamia nyumba ya kupanga,” ameeleza Sajid.
Zaidi ya kazi yake, Sajid ameongoza filamu kama vile ‘Heyy Babyy’, ‘Darna Zaroori Hai’ na ‘Himmatwala’. Licha ya mabishano hayo, Sajid anajaribu kusonga mbele.




