Twiga Stars ilitikisa 2024

DAR ES SALAAM: MIONGONI mwa matukio yasiyosahaulika mwaka huu ni pamoja na kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Timu ya Taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars kwa mara ya pili baada ya miaka 13.
Kikosi cha Twiga Stars kimeweka historia baada ya kujinyakulia nafasi ya kushiriki michuano ya Wafcon kwa mara ya pili kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2 dhidi ya timu ya Taifa ya wanawake ya Togo.
Twiga Stars imejihakikishia nafasi kwenye kombe la Wafcon kwa wanawake licha ya kupoteza 1-0 ugenini dhidi ya Togo, tayari walikuwa kifua mbele kwa mabao 3-0 kufuatia ushindi wao wa awali wa nyumbani mechi iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Wachezaji wote walifanya vizuri wakiongozwa na washambuliaji Opa Clement anayekipiga China na Aisha Masaka anayekipiga kwa sasa Brighton ya Uingereza walioonesha kiwango bora.
Kabla ya kufuzu kumenyana na Togo, Tanzania iliibuka na ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Ivory Coast kwa njia ya penati baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.
Kuwepo kwa wigo mkubwa wa wachezaji wa kike kucheza soka la kulipwa nje imesaidia kwa Tanzania kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ikiwemo hiyo ya kufuzu WAFCON.
Haikuwa rahisi kulingana na ubora wa wapinzani lakini malengo yalitimia ya kujenga heshima katika nchi. Fainali za Wafcon zilitarajiwa kufanyika mwaka 2024 na kusongezwa mbele kuchezwa 2025 nchini Morocco.
Mara ya mwisho Stars kufuzu fainali hizo kwa wanawake ilikuwa 2010 ilipofungwa dhidi ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 4-0, miongoni mwa wachezaji waliofanikisha fainali hizo ni Ester Chambruma, Kocha Mkuu wa JKT Queens na Sophia Mwasikile kwa sasa meneja wa kikosi cha Simba Queens, timu zote zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
FURAHA KUTAWALA:
Tanzania ilifurahi na kupitia Rais wa nchini, Samia Suluhu Hassan alituMa salamu za pongezi kwa vijana hao na alitoa zawadi ya Sh Million 10.
Ikumbukwe siku Twiga Stars inafuzu, Rais Samia alimuapisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ambapo sasa hivi imeongezeka na Habari pamoja na msemaji wa Serikali.