Ndimbo :Hatutakiwi kuhesabu vidole kufuzu Afcon

OFISA Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ‘TFF’, Clifford Ndimbo amesema kikosi cha Taifa Stars kimeingia kambini kujiandaa na michezo miwili dhidi ya Ethiopia na Guinea.
Amesema michezo hiyo ni muhimu kuvuna alama sita kwa ajili ya kutoa mwanga wa kufuzu au kutofuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, zitakazofanyika nchini Morocco.
“Timu imeanza kuingia kambini kwa wachezaji wa ndani, wanaocheza nje watajiunga mapema na kuungana na nyota waliopo kambini kujiandaa na michezo hiyo ya maamuzi. Tunalazimika kufanya vizuri na kushinda mechi ya ugenini dhidi ya Ethiopia tutakayocheza nchini DR Congo, baadae tutacheza nyumbani dhidi ya Guinea, “ amesema.
Ndimbo amesema wanalazimika kushinda ili kukusanya alama sita na kufuzu kucheza fainali hizo na endapo watapoteza hata pointi moja watakuwa katika kipindi kigumu na kupelekea kuhesabu vidole.
Tanzania ipo nafasi ya tatu kwenye Kundi H linaloongozwa na DR Congo, Guinea akishika nafasi ya pili huku Ethiopia wakiburuza mkia.




