BurudaniFilamu

KUMSHUHUDIA mtu unayempenda sana akiwa hoi kitandani ni jambo gumu mno, unaweza
kutamani ulale wewe ili yeye aamke, japo umpunguzie maumivu.

Mwanamume anayeitwa Ray Cooper anampambania mkewe, Amanda Cooper, ambaye yupo hoi kitandani kutokana na maradhi ya saratani yanayomsumbua kwa muda mrefu.

Ni mwanamume ambaye anatamani afanye kila linalowezekana ili mkewe apone ila wenye madaraka na fedha, kwa tamaa zao za kifedhuli, wanamwalika zilaili, malaika mtoa roho,
kwenye kitanda cha mkewe ili kuichukua pumzi yake.

Mambo haya yasikie kwa wengine tu, usiombe yakukute kwani inaumiza sana kiukweli!
Ray Cooper anaambiwa kuwa dawa pekee ya kumwokoa mkewe ni moja tu, dawa ambayo inatengenezwa na kampuni ya BioPrime lakini tatizo ni kwamba gharama ya dawa hii ni kubwa mno.

Ray Cooper anajitahidi sana kwa kadiri ya uwezo wake ili afanikiwe kuipata dawa hii lakini anashindwa na sasa yupo mbioni kumpoteza mkewe.

Ila leo kuna habari njema zinamfikia baada ya kuambiwa kwamba kuna dawa mpya ya bei nafuu na ya uhakika inayoweza kumwokoa mkewe itaingia sokoni wakati wowote.

Dawa hii ina ufanisi mkubwa kama dawa ile ile inayotengenezwa na BioPrime ila hii ya sasa
imetengenezwa kwa kuzingatia uwezo mdogo wa kifedha kwa watu maskini.

Ray Cooper na binti yake Rachel mwenye umri wa miaka 18 wanaungana na wanafamilia wengine kusherehekea habari hii njema kuhusu ujio wa dawa mpya ambayo hatimaye itamponya mkewe.

Lakini katika hali ya kushangaza, siku chache tu kabla Amanda hajaanza matibabu Ray Cooper anapokea taarifa mbaya kuwa dawa hizi alizokuwa akizisubiri kwa hamu kubwa hazitapatikana tena, na watengenezaji wa dawa hizi “eti” wameamua kuziondoa sokoni kwa muda usiojulikana!

Subiri kwanza! Ni nini kimetokea? Ni nini kimesababisha hali hii? Je, Ray Cooper atafanya nini kumwokoa mkewe anayekaribia kufa? Habari za chini ya zulia ni kwamba kampuni ya
BioPrime imenunua dawa zote na umiliki wake toka kwenye kampuni inayotengeneza
dawa hizo lengo lao likiwa wao ndio wazalishe na kuziuza dawa hizi mpya.

BioPrime wanafanya hivi kwa kuwa wanadhani kuwa endapo dawa hizi za bei nafuu zikiingia sokoni wao hawataweza kuuza dawa zao.

Kwao, ni heri punda wafe lakini mzigo ufike! Wakati Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya BioPrime, Simon Keeley akiwa kwenye runinga kuelezea dawa za kampuni yake, Ray Cooper anapiga simu na kutishia kumuua endapo mkewe atakufa.

Simon Keeley hajali kuhusu vitisho vya Ray Cooper, na siku chache baadaye Amanda anakufa kwa sababu Ray Cooper ameshindwa kununua dawa ambazo gharama yake ni kubwa sana, na zile alizozitarajia, za bei nafuu, zimezuiwa kuingia sokoni.

Sasa Ray Cooper anapitia kipindi kigumu sana, na kujaribu kusahau jambo hili ni vigumu
mno hasa baada ya  kumzika mkewe.

Miezi sita baadaye anapokea simu kutoka kwa mwandishi wa habari ambaye anajitambulisha kwa jina la Martin Bennett, na anamwomba wakutane, kisha anamwambia kuwa anao ushahidi kuhusu udhalimu wa kampuni ya BioPrime uliofanyika katika kuziondoa sokoni zile dawa za bei nafuu.

Mwandishi huyu anaonekana kuyajua mengi ya kidhalimu yanayoendelea kwenye kampuni
ya BioPrime, na kwamba wamekuwa wakimhonga yeyote anayejaribu kuhoji  kuhusu udhalimu wao.

Lakini kabla hajafunguka zaidi anauawa pale pale. Inaonekana kuna jambo kubwa sana limejificha nyuma ya pazia, na sasa Ray Cooper anaamua kulivaa jambo hili ‘mazima’
kutafuta mchawi ni nani!

Anaanza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa BioPrime, Simon Keeley anayemwambia hajui
chochote na kumtaka aende kwa mwenyekiti wake, Vinod Shah. Baada ya mapambano
makali sana yanayomwacha mmoja wa walinzi wa Simon Keeley akiwa mfu, Ray Cooper anamnyonga Simon Keeley kwa kutumia mfuko wa plastiki.

Sasa Ray Cooper anagundua kuwa kulikuwa na udhalimu mkubwa uliokuwa unafanyika kwenye kampuni ya BioPrime na wamiliki wake wametajirika kwa kiwango kikubwa sana kutokana na udhalimu huo.

Mbaya zaidi, udhalimu huo unafahamika mpaka serikalini na wapo baadhi ya viongozi wakubwa serikalini ambao wanashiriki katika udhalimu huo. Sasa msako wa kumtafuta
mchawi unakolea.

Ni aksheni kwa kwenda mbele, na Ray Cooper anaonesha makali yake. Mwishowe
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) wanamweka mtu kati lakini anafanikiwa kuwatoka na kurukia kwenye paa la uwanja wa baseball.

Mpelelezi wa FBI, Sarah Meeker anamtaka Ray Cooper ajisalimishe na ndipo inapogundulika kuwa mtu anayedhani ni Ray Cooper, si yeye bali ni Rachel, binti yake. Kimsingi Ray Cooper aliuawa siku ile ile ambayo mwandishi Bennett aliuawa!

Dah! Ni vipi Rachel ameweza kuyafanya yote hayo kwa kutumia sura ya baba yake? Unaambiwa ukitaka kuujua uhondo wa ngoma ingia ucheze… Ukiitazama filamu hii kwa umakini utagundua kuwa hakuna biashara nzuri kama ya tiba yaani jambo lolote la afya sehemu yoyote ile ni biashara nzuri.

Lakini hakuna kitu kibaya zaidi kama biashara hii itamilikiwa na watu wakubwa serikalini wasio na maadili. Filamu hii ya dakika 110 iliachiwa kwenye mtandao wa Netflix mnamo Agosti 20, 2021. Imeandikwa na Phillip Eisner na Gregg Hurwitz na imeongozwa na Brian Andrew Mendoza.

Sms: 0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

 

Related Articles

Back to top button