Chemical atimiza ndoto sasa ni Dk Lubao

ENGLAND:MSANII wa muziki wa hip-hop kutoka Tanzania, Claudia Lubao maarufu kama Chemical, ameandika historia mpya baada ya kufaulu mtihani wake wa mwisho wa shahada ya uzamivu (PhD) na sasa anafahamika rasmi kama Dk Lubao.
Chemical alihitimu shahada hiyo katika Chuo Kikuu cha St Andrew, nchini Uingereza. Kabla ya kujiunga na chuo hicho kwa ufadhili wa kimasomo, alikuwa tayari amefanya vyema kitaaluma akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako alisoma shahada ya kwanza ya Sanaa za Maonesho, na baadaye shahada ya uzamili katika Usimamizi wa Urithi wa Kitamaduni.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Chemical aliandika ujumbe wa shukrani uliogusa wengi akisema:
“Nilikuwa na ndoto, na leo nimeamka kama Dk Lubao!”
Amewashukuru wasimamizi wake, idara mbalimbali, jopo la watahini, marafiki, pamoja na mashabiki waliomsapoti katika safari yake ya kitaaluma.
Chemical ambaye amejizolea umaarufu kwa nyimbo zenye ujumbe mzito wa kijamii, ameendelea kuthibitisha kuwa inawezekana kuwa msanii na pia kung’ara katika elimu ya juu.
Shahada yake ya uzamivu inahusiana na urithi wa kitamaduni na mchango wa muziki wa kizazi kipya katika kuwasilisha masuala ya kijamii kama mabadiliko ya tabianchi.
Hii ni hatua ya kipekee, si tu kwa safari yake binafsi bali pia kwa wasanii wengine wanaotamani kuunganisha sanaa na taaluma. Kwa sasa, mashabiki wake wanampongeza kwa mafanikio haya makubwa huku wakingoja kwa hamu kazi zake mpya zenye ladha ya utafiti na uelewa wa kina.