
DODOMA: MBUNGE wa Shaurimoyo, Ali Juma Mohamed, amepongeza kurejeshwa kwa Ligi ya Muungano, akisema ni hatua muhimu katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji vya michezo.
Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Muungano na Mazingira leo Aprili 25, Ali amesema michezo imekuwa sehemu muhimu ya harakati za kuleta umoja, kuanzia enzi za kupigania uhuru hadi kufanikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Michuano ya Kombe la Muungano ya mwaka huu inaendelea katika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba, ikiwa ni msimu wa pili mfululizo tangu kurejeshwa kwake mwaka 2024 baada ya kusimama kwa zaidi ya miongo miwili. Timu nane zinashiriki michuano hiyo — nne kutoka Tanzania Bara na nne kutoka Zanzibar — zikionesha ushindani wa hali ya juu na hamasa kubwa ya mashabiki.
Mbunge, Ali Juma alitaja baadhi ya wachezaji waliotokea Unguja ambao wamefanikiwa kitaifa kama Feisal Salum ‘Feitoto’, Ibrahim Hamad ‘Sajenti Bacca’ na Mudathir Yahya Abbas, kuwa ni mifano hai ya vipaji vinavyoweza kuinuliwa kupitia uwekezaji kwenye michezo. Alisisitiza kuwa Ligi ya Muungano ni zaidi ya mashindano, bali ni chombo cha kuimarisha undugu wa pande mbili za Muungano.
Awali, michuano hiyo ilipangwa kufanyika Uwanja wa New Amaan Complex, lakini ilihamishiwa Gombani kufuatia ushauri wa kiufundi kutoka CAF ili kulinda ubora wa uwanja huo mpya. Nusu fainali zinatarajiwa kuchezwa Aprili 28 na 29, huku fainali ikipangwa kufanyika Mei Mosi, 2025.
Kwa mujibu wa Bunge na wadau wa michezo, kurejea kwa michuano hii si tu heshima kwa historia ya Muungano bali pia ni jukwaa la kuwaunganisha Watanzania kupitia lugha ya michezo na kuibua vipaji vitakavyoiwakilisha nchi kitaifa na kimataifa.