Africa

Yanga vs Rivers United: Ni mechi ya kisasi

YANGA imemjua mpinzani wake Rivers United ya Nigeria baada ya kufanyika kwa droo
ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, wakipokea tabasamu usoni na imani mioyoni mwao wakiamini wanakwenda kulipa kisasi.

Wanataka kulipa kisasi kwa sababu walijeruhiwa mnamo mwaka juzi walipokutana kwenye raundi ya awali na Yanga kupoteza katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa
kichapo cha bao 1-0 nyumbani na ugenini 1-0.

Mtazamo wa Wanajangwani wanaamini kwa kipindi kile walichokutana hawakuwa vizuri na tena kwa sababu kulikuwepo wa virusi vya corona kulitokea mtafaruku walipokwenda
Nigeria katika mchezo wa mkondo wa pili.

Ilikuwa hivi, baadhi ya wachezaji wa Yanga walitajwa kuwa na virusi vya corona hivyo Yanga ikagoma na kugombana nao wakisema ni figisu za kuwazuia wachezaji wao wasicheze, lakini baadaye walisuluhisha mambo yakaenda sawa.

Pia, kuna wachezaji kadhaa hawakuwepo kipindi kile kama Khalid Aucho, Fiston Mayele na wengine wengi na sasa wanakutana na Yanga ambao mwaka huu wameuanza msimu vizuri
wakiwa na kikosi chenye ushindani na matamanio ya kufika mbali.

SAFARI ZAO
Yanga imemaliza Kundi D ikiwa kinara kwa kufikisha pointi 13 baada ya kucheza michezo sita, kushinda minne, sare moja na kupoteza mmoja.

Ni rekodi ya kipekee wameiweka msimu huu ukilinganisha na miaka mingine waliyowahi kufika hatua ya makundi huko nyuma ambako walikuwa wanafungwa na hata kumaliza kundi katika nafasi ya tatu na nne.

Mshindi wa pili alikuwa ni US Monastir ya Tunisia waliolingana pointi, wakifuatiwa na Real Bamako ya Mali yenye pointi tano na TP Mazembe ikishika mkia kwa pointi tatu.

RIVERS UNITED
Rivers United ilikuwa Kundi B na ilimaliza katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 10 nyuma ya vinara, Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyokuwa na pointi 13. Katika michezo sita waliyocheza walishinda mitatu, sare moja na kupoteza miwili.

Walikuwa na Diables Noirs ya Congo iliyokuwa katika nafasi ya tatu kwa pointi sita na Motema Pembe ya DRC pointi tatu.

Takwimu za timu hii zilipokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani zimeonesha walikuwa moto na wala hawapaswi kubezwa, walishinda mabao 3-0 dhidi ya Asec Mimosas, wakashinda mabao 3-1 dhidi ya Motema Pembe na kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Diables Noirs.

Rivers walishinda mechi moja ya ugenini bao 1-0 dhidi ya Motema Pembe. Katika mechi ya mtoano kuingia hatua ya makundi walicheza na Wydad Casablanca ambapo wakiwa
nyumbani kwao walishinda mabao 2-1 kisha ugenini Morocco walipigwa 6-0. Ni timu yenye uwezo wa kufunga mabao.

Timu hiyo ina mshambuliaji hatari anaitwa Paul Acquah kutoka Ghana ambaye alifunga mabao manne kwenye hatua ya makundi, mchezo mmoja alifunga ‘hat trick’ dhidi ya Motema Pembe nyumbani na lingine moja ugenini.

Rivers ina wachezaji wanane wa kigeni na kati ya hao wanne wanatoka Ghana, mmoja Ivory Coast, mmoja Cameroon na wawili wanatoka Liberia huku asilimia kubwa ya kikosi chao wakiwa ni wazawa.

Pamoja na uchanga wao kwenye michuano ya Afrika ni timu ambayo inajitahidi kwa kiasi fulani. Rekodi zao zinaonesha timu hiyo iliyoundwa mwaka 2016, imeshiriki Ligi ya Mabingwa mara mbili mwaka 2017, ilitolewa hatua za awali na mwaka 2022 ilitolewa
raundi ya pili.

Mwaka 2017 baada ya kutolewa raundi za awali, waliangukia kwenye Kombe la Shirikisho na kufanikiwa kuishia hatua ya makundi ikiwa bado ni timu changa kwa hiyo hayo yalikuwa
mafanikio makubwa kwao.

Mwaka 2020/2021 walitolewa kwenye mchezo wa mwisho wa mtoano na kushindwa kuingia hatua ya makundi.

Msimu huu wamevunja rekodi kwa sababu ni mara ya kwanza wanaingia hatua ya robo fainali ikionesha dhahiri na wao wanataka mafanikio zaidi na wamejitahidi hadi hapo walipofikia wakionesha ushindani kwa timu kongwe walizocheza nazo hatua ya makundi.

Rivers ni kama Yanga, walianzia Ligi ya Mabingwa wakatolewa kwenye mtoano na kuangukia Kombe la Shirikisho.

Ukiacha rekodi hiyo, mwaka jana walishinda taji lao la kwanza Ligi Kuu Nigeria tangu kuitwa Rivers kwa sababu ni klabu iliyoundwa kwa kuunganisha timu mbili za Dolphin na Sharks FC.

Baada ya ushindi huo wachezaji na maofisa wao walizawadiwa dola za Kimareni 20,000 zaidi ya Sh milioni 46 kila mmoja na serikali ya Jimbo la Rivers.

Pia, waliahidiwa dola za Kimarekani 40,000 nyingine ikiwa wangefuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa sawa na zaidi ya Sh milioni 93 lakini kwa bahati mbaya waliangukia Kombe la Shirikisho na kufuzu huku.

YANGA V RIVERS
Mchezo wa kwanza Yanga itakuwa ugenini Nigeria Aprili 23, mwaka huu kisha watarudiana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Aprili 30. Mechi ya Yanga na Rivers haitakuwa nyepesi kama wanavyofikiria baadhi yao, kwa sababu kila mmoja atataka kuweka rekodi mpya.

Pamoja na uzoefu wa muda mrefu wa Yanga haimaanishi kwamba ni rahisi kufuzu, lazima wapambane kufa au kupona. Inachukuliwa kama timu rahisi lakini inaweza kuleta
changamoto kwa Yanga kwani nao wana wachezaji wazuri.

Siku zote inajulikana mataifa ya Magharibi mwa Afrika yana vipaji vikubwa. Nchi ya Nigeria
na Ghana zimejaliwa vipaji. Takwimu za mechi ya hatua ya makundi zimeonesha wazi kwamba sio timu inayopaswa kubezwa bali Yanga inatakiwa kuwaheshimu na kujipanga dhidi yao.

Kila mmoja anaweza kuchukua tahadhari na isitoshe Rivers tayari waliwahi kuja kucheza na Yanga Tanzania na kule kwao hivyo wanajua aina ya mpinzani wanayekwenda kukutana
naye.

Yanga inaweza kufuzu hatua ya nusu fainali kutegemea na itakavyojiandaa dhidi ya mwenzake kwa kutowadharau wapinzani bali kuwaheshimu na kujipanga na hapo ndipo
kaulimbiu yao ya kisasi ni haki itakapotimia.

Related Articles

Back to top button