Yanga, UNICEF kushirikiana elimu UVIKO, Ebola

KLABU ya Yanga leo imeingia mkataba wa ushirikiano wa miezi sita na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) unaolenga kuongeza uelewa kwa umma kuhusu Chanjo ya UVIKO-19 na uhamasishaji kuhusu virusi vya EBOLA.
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa Habari Dar es Salaam, Rais wa klabu hiyo Injinia Hersi Said amesema mkataba huo utaanza rasmi Oktoba 23 wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya Simba katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Ni jukumu letu kama Klabu kuunga mkono juhudi zitakazotuwezesha kushinda UVIKO-19 na Ebola,” amesema Hersi.
Amesema hiyo ni mara ya kwanza katika historia kwa vilabu vya Afrika Mashariki na kwamba ushirikiano na UNICEF umejengwa katika falsafa ya Klabu ya kusaidia jamii.
Naye Mwakilishi wa UNICEF Tanzania Fatimata Baladi amesema kutokomeza magonjwa ya milipuko kama vile UVIKO-19 na Ebola kunahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa wadau katika nyanja mbalimbali.
“Ushirikiano wetu utasaidia zaidi ya mashabiki milioni 25 wa soka nchini Tanzania kupata taarifa sahihi kuhusu chanjo ya UVIKO-19 na virusi vya Ebola ili waweze kujilinda,” amesema Baladi.
Septemba 20, 2022 serikali ya Uganda ilitangaza mlipuko wa virusi vya Ebola katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo ambapo kufuatia hali hiyo Tanzania imekuwa katika juhudi kuhakikisha virusi hivyo haviingii hapa nchini.