Africa

YANGA mguu sawa kimataifa

YANGA kesho inaanza kibarua chake cha kusaka ushindi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Association Sportive d’Ali Sabieh Djibouti Telecom (ASAS FC) ya Djibouti utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Yanga wanaingia katika michuano hiyo wakiwa na malengo ya kufanya vizuri zaidi hasa baada ya kushindwa kufika hatua za juu katika mashindano hayo.

Lakini inajivunia kufika fainali yake ya kwanza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) msimu uliopita, ambapo walishindwa kuchukua taji baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya US Alger ya Algeria.

Kilichompa mpinzani wake ushindi ni kwa sababu ya mabao mengi ya ugenini aliyoshinda Dar es Salaam 2-1 kisha kwao wakafungwa 1-0. Huu ni msimu mpya watu wanataka kujua Yanga wamerudi vipi, wataweza kuwa katika ubora ule ambao ulionekana msimu uliopita?

Yanga ya sasa haina mshambuliaji hatari kama Fiston Mayele aliyeibuka mfungaji bora wa Cafcc aliyeuzwa Pyramids ya Misri, haina Yanick Bangala aliyeuzwa Azam FC wala Djuma Shabani na wengine wengi walioondoka baada ya mikataba yao kuisha.

Wala haina Kocha Nasreddine Nabi aliyeipa timu hiyo mafanikio makubwa ya taji la Ligi Kuu na kuifikisha timu hiyo kwenye fainali.

YANGA MPYA
Yanga ya msimu huu ina Kocha mpya, Miguel Gamondi raia wa Argentina mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika. Ina baadhi ya wachezaji wapya ambao tayari wameonesha kiwango katika michuano ya Ngao ya Jamii.

Kuna wachezaji kama Kouassi Attohoula na Pacome Zouzou kutoka Asec Mimosas, Nickson Kibabage (Singida Big Stars), Jonas Mkude (Simba), Maxi Nzengeli (As Maniema), Hafiz Konkoni kutoka Bechem United ya Ghana.

Usajili huo sambamba na wale wazoefu waliopo kwenye kikosi hicho wanatarajiwa kuisaidia timu kwenye mashindano hayo makubwa Afrika. Tayari wamecheza michezo kadhaa ya kirafiki ya kimataifa na Ngao ya Jamii wameonesha ni namna gani wamejiandaa kufanya vizuri.

Walicheza dhidi ya Kaizer Chief ya Afrika Kusini na kushinda bao 1-0 siku ya Mwananchi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, walicheza dhidi ya Azam FC wakashinda mabao 2-0
Mkwakwani Tanga kisha kutoka suluhu dhidi ya Simba na baadaye kutolewa kwa mikwaju ya penalti 3-1.

Wamefanya maandalizi ya kutosha ya msimu wakiwa katika kambi yao ya Avic Town Kigamboni kwa muda mrefu na Kocha wao Gamondi tayari anaonekana kuwateka wachezaji kwa mbinu zake za mpira wa pasi na kasi baada ya kuonesha kiwango bora katika michezo kadhaa iliyopita.

YANGA VS ASAS
Huu ni mchezo muhimu kwa Yanga kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo wa kwanza kisha kusubiri wa marudiano utakaochezwa kwenye uwanja mmoja wa Azam Complex na kushinda ili kutinga raundi ya pili ya awali.

Endapo Yanga ataiondoa ASAS, basi atatinga hatua inayofuata ambapo atacheza na mshindi wa mchezo utakaozikutanisha AS Otoho ya Congo na El Merrikh ya Sudan. Yanga inahitaji juhudi kama kweli inataka kuingia hatua ya makundi.

Kama itafanya vizuri katika mechi hizo mbili, basi itajihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya
makundi. Akitolewa hatua za awali, awamu hii hataangukia Kombe la Shirikisho kama
ilivyozoeleka kwani utaratibu umebadilika na badala yake watarudi nyumbani na kuendelea na mashindano ya kitaifa.

Wanakutana na timu ya Asas sio timu ya kubezwa, wanafanya vizuri katika ligi yao, wamesajili na wana matumaini na malengo kama ilivyo kwa Yanga kwa hiyo wajiandae na kuwaheshimu wapinzani wao ili kufanya vizuri.

Asas ni klabu iliyoanzishwa mwaka 1991, inamiliki Uwanja wa El Hadj Hassan Gouled Aptidon, wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 20,000. Imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Djibouti mara saba na Djibouti Cup mara tatu, ndio klabu iliyofanikiwa zaidi nchini humo, lakini soka lao haliko juu ukilinganisha na letu.

Timu hii haijawahi kuvuka hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa wala Kombe la Shirikisho barani Afrika hivyo, wanatafuta historia ya kufanya vizuri. Msimu uliopita ilishiriki
Kombe la Shirikisho ikatupwa nje hatua ya awali kwa kufungwa bao 1-0 na AS Kigali ya Rwanda.

Kwa kuwa uwanja wao haukukidhi vigezo vya Caf, timu hiyo imelazimika kucheza mechi yake ya nyumbani katika Uwanja wa Azam Complex. Ni timu inayoonekana kuwa na ushindani japo kwa kiasi lakini sio ya kutisha sana.

Ingawa kwenye mpira siku zote hupaswi kubeza timu ndogo maana nazo zinajipanga kuonesha maajabu yake na kutafuta historia. Kikosi cha Asas kina mchezaji aliyewahi kuchezea Yanga, Yacouba Songne hivyo huenda akawapa uzoefu wake wenzake na kuisaidia timu yao kufanya vizuri.

Bado Yanga ina nafasi zaidi ya kufanya vizuri kwa sababu kwanza ni wazoefu wa mashindano ya kimataifa, wana kikosi kizuri chenye ushindani na wanatumia uwanja ambao wameuzoea.

Yanga iliwahi kutumia uwanja huo mara kadhaa katika michezo tofauti na kupata matokeo hivyo, mashabiki wa soka Tanzania wana imani kwamba watafanya vizuri na kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Baada ya mchezo huo wa kwanza timu hizo zitarudiana tena Agosti 28 na mshindi wa mechi hii anatarajia kukutana na mshindi kati ya Ottoho ya Congo au Al Merreikh ya Sudan.

RAUNDI YA PILI
Yanga watakapovuka hatua hiyo ya kwanza ya awali, watacheza raundi ya pili ya awali dhidi ya mshindi kati ya AS Otoho na El Merrikh, hapo timu hiyo ya Sudan ndio inaweza kuleta upinzani mkubwa kwa Yanga kwani ina uzoefu na mechi za kimataifa.

El Merrikh ni moja ya klabu kongwe kabisa barani Afrika baada ya kuanzishwa mwaka 1908 na sasa ina takribani miaka 115 tangu kuanzishwa kwake na imewahi kutwaa Kombe la
Washindi Afrika mwaka 1989 huku ikimaliza ya pili katika Kombe la Shirikisho mwaka 2014.

Timu hiyo pia imetwaa mara tatu taji la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) mwaka 1986, 1994 na 2014, hivyo sio timu ya kuibeza.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button