YANGA HAICHEKESHI!

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga imeonesha ubora wake kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao 7-1 dhidi ya Polisi Tanzania na kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho. Mchezo huo ulipigwa jana katika Uwanja wa KMC Complex uliopo jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Yanga ilianza kwa kasi kubwa na kuonesha kandanda la kuvutia lililowafanya mashabiki waliojitokeza uwanjani kushuhudia mvua ya mabao. Tangu dakika za mwanzo, timu hiyo ilitawala mchezo kwa pasi za uhakika na mashambulizi ya mara kwa mara yaliyoisumbua safu ya ulinzi ya Polisi Tanzania.
Nyota wa mchezo huo alikuwa mshambuliaji Aurelia Depu aliyefunga mabao matatu (hat-trick) na kuendelea kuonesha makali yake langoni. Mabao mengine ya Yanga yalifungwa na Mudathir Yahya, Buba Jameh na Abdulnasir Mohamed huku bao lingine likitokana na beki wa Polisi Tanzania Joseph Majagi aliyejifunga wakati akijaribu kuokoa hatari langoni mwao. Polisi Tanzania walipata bao lao baada ya beki wa Yanga Frank Asink kujifunga katika dakika ya 81 ya mchezo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Yanga Pedro Goncalves amesema ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake, akieleza kuwa alitumia nafasi hiyo kuwapa dakika baadhi ya wachezaji ambao hawapati nafasi mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.
“Lengo lilikuwa kuwapa nafasi wachezaji wengine ili kuongeza ushindani ndani ya kikosi. Nafurahi kuona kila aliyepata nafasi ameonesha kiwango kizuri na timu inaendelea kuimarika kadri michezo inavyokwenda,” amesema kocha huyo.
Ushindi huo unaipa Yanga morali kubwa kuelekea hatua inayofuata ya huku ikiwa na matumaini ya kuendelea kufanya vizuri na kutwaa tena taji la michuano hiyo msimu huu.




