Writz avunja rekodi Liverpool

LIVERPOOL, Mabingwa wa ligi kuu ya England Liverpool wamefanikiwa kumsajili kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Ujerumani Florian Wirtz kutoka kwa klabu ya Bundesliga Bayer Leverkusen kwa dau lililovunja rekodi yao ya uhamisho la Pauni milioni 116.
Leverkusen itapokea kitita cha pauni milioni 100 (Bilioni 352.56 za kitanzania) na nyongeza ya pauni milioni 16(Bilioni 53.28 za Kitanzania) kama bonasi ikiwa mchezaji huyo atafanya vizuri katika klabu yake mpya.
Hii inamfanya mchezaji huyo wa Liverpool mwenye umri wa miaka 22 kuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kutokea klabuni hapo, mbele ya beki wa kati wa Uholanzi na nahodha Virgil van Dijk ambaye alijiunga kwa pauni milioni 75 mwaka 2017.
Wirtz, ambaye amesaini mkataba wa miaka mitano, pia anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa kwa pauni milioni 100 katika historia ya Ligi Kuu ya England, akiungana na viungo wa Chelsea Enzo Fernandez na Moises Caicedo, Declan Rice wa Arsenal na winga wa Manchester City Jack Grealish.
“Ninajisikia furaha na fahari sana. Hatimaye jambo nililokuwa nikilisubiri muda mrefu limekamilika. Nimefurahia sana kuanza safari mpya na nzuri iliyo mbele yangu.”
“Hili pia lilikuwa jambo kubwa sana kwenye mawazo yangu, ninekuwa nikitamani kuwa na kitu kipya kabisa, kuondoka Bundesliga na kujiunga na Ligi Kuu ya England.” Wirtz alisema katika taarifa yake.
Wirtz aliisaidia sana Leverkusen, na kuwaongoza kutwaa ubingwa wa Bundesliga bila kufungwa hata mchezo mmoja vilevile kutwaa kombe la ligi maarufu kama DFB Pokal wa 2023-24 huku wakienda misimu miwili ya ligi bila kupoteza ugenini.
Mjerumani huyo alifunga mabao 57 na kutoa pasi za mabao 65 katika mechi 197 alizoichezea Leverkusen, baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea Cologne mwaka 2020. Alifunga mabao 16, huku akitoa pasi za mabao 15, katika mechi 45 msimu uliopita Leverkusen ikimaliza nafasi ya pili nyuma ya Bayern.




