Wissa njiapanda Brentford

LONDON: MENEJA wa Brentford Keith Andrews amethibitisha Fowadi wake Yoane Wissa hatakuwepo katika mechi ya Jumapili ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Nottingham Forest kwa sababu hana uhakika juu ya mustakabali wake klabuni hapo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa DR Congo mwenye umri wa miaka 28 amevutia klabu kadhaa za ligi hiyo zikiwemo Nottingham Forest na Newcastle United.
Mechi ya kwanza ya ligi ya Andrews inakuja baada ya kikosi hicho kutikiswa kwenye dirisha hili la usajili ambapo meneja wao wa muda mrefu Thomas Frank alijiunga na Tottenham Hotspur, na wachezaji muhimu wakaondoka.
Brentford waliomaliza katika nafasi ya 10 msimu uliopita, walimuuza mfungaji wao bora Bryan Mbeumo kwenda Manchester United na nahodha wao Christian Norgaard akahamia Arsenal.
“Nimefanya uamuzi kuwa hatakuwepo. Maandalizi yetu ya msimu mpya yamevurugwa sana na nia ya Yoane kuondoka iko wazi. Kama kocha mkuu nataka Yoane awepo na awe sehemu ya kikosi cha kwanza. Lakini ninaelewa nia yake. Nina uhusiano mzuri nae, na hilo litaendelea, lakini tunataka abaki.” – alisema Andrews.