
DAR ES SALAAM:MSANII wa filamu na Mkurugenzi wa Taasisi ya Wema wa Mama, Wema Sepetu, maarufu kama Tanzania Sweetheart, ameomba radhi kwa kuvaa nguo zisizo na maadili na kuahidi kuwa tukio hilo halitajirudia tena.
Akizungumza baada ya kuitikia wito wa Bodi ya Filamu Tanzania, kufuatia picha zake zilizozua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii, Wema amesema kikao hicho hakikuwa cha kisheria, bali cha kukumbusha kuhusu maadili ya wasanii.
“Nilikuja Bodi ya Filamu kuitikia wito. Kikao hakikuwa rasmi, bali kilikuwa cha kukumbushana juu ya maadili. Nimeyasikia na nimeyazingatia,” alisema Wema.
Ameongeza kuwa anakiri kufanya kosa, lakini amejifunza kupitia mkutano huo na sasa anatambua vyema nafasi yake kama mtu mwenye ushawishi mkubwa katika jamii.
“Kufanya kosa si kosa, bali kurudia kosa ndio kosa. Nachukua nafasi hii kuomba msamaha kwa wote niliowakwaza. Nimejifunza, na haitajirudia tena,” amesisitiza.
Wema pia amewaomba radhi mashabiki wake na wale wanaomchukulia kama kioo cha jamii, akiwahakikishia kuwa atakuwa makini zaidi na mwenendo wake katika siku zijazo.
“Niwashukuru Bodi ya Filamu kwa upendo wao. Nimejifunza kuwa nafasi yangu ni kubwa sana katika jamii. Naomba msamaha kwa wote niliowakwaza,” aliongeza kwa unyenyekevu.
Tukio hili limezua mijadala mbalimbali kuhusu wajibu wa wasanii kama viongozi wa maadili na tabia katika jamii.