KOCHA Mkuu wa Polisi Tanzania Mwinyi Zahera amesema timu hiyo ilishindwa kupata matokeo mzuri kwenye mechi zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na wachezaji kukata tamaa.
Akizungumza na SpotiLeo kocha huyo aliyeteuliwa hivi karibu kukikonoa kikosi hicho amesema atatumia mbinu zake kuhakikisha anawajenga wachezaji kisaikolojia ili kupandisha ari ya kupambana kwa lengo la kufanya vizuri.
Zahera amesema pia atatumia dirisha dogo kufanya usajili wa nguvu ili kuirudisha timu hiyo kwenye ushindani.
“Timu siyo mbaya sana inahitaji marekebisho madogo ikiwemo kuimarisha safu ya ushambuliaji na ulinzi,” amesema Zahera.
Kwa mujibu wa kocha huyo muda wa wiki moja aliyokaa na timu hiyo amebaini mapungufu eneo hilo hivyo atahakikisha unafanyika usajili sahihi wa wachezaji watakaoimarisha timu.
Zahera amesaini mkataba wa miezi sita kuifundisha Polisi iliyokuwa ikinolewa na kocha msaidizi John Tamba ambaye kwa sasa ni msaidizi wa Zahera.
Polisi Tanzania imemaliza msunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushika nafasi ya 16 mwisho wa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 9 baada ya michezo 15.




