Wachezaji Chess Tanzania wajipanga Kombe la Dunia

DAR ES SALAAM: CHAMA cha mchezo wa Chess Tanzania kimesema kimeanza maandalizi ya kushiriki mashindano makubwa ya dunia yanayofanana na Olimpiki yanayotarajiwa kufanyika nchini Uzbekistan kati ya Septemba na Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na SpotiLeo kuhusu maandalizi hayo, msemaji wa chama hicho Mussa Mangula amesema wanatarajia kuandaa mashindano ya Taifa ya Chess yatakayofanyika Mei Mosi mwaka huu kwa lengo la kupata kikosi bora kitakachoiwakilisha Tanzania.
Mangula amesema mashindano hayo ya kitaifa yatatumika kama hatua ya kuchuja wachezaji watakaoingia kwenye timu ya taifa itakayoshiriki mashindano ya Chess Olympiad, yanayotarajiwa kushirikisha zaidi ya mataifa 100 kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Amesema chama hicho kinafanya maandalizi ya kina ili kuhakikisha wachezaji watakaopatikana wanakuwa na uwezo wa kushindana katika kiwango cha kimataifa.
“Tunajiandaa vizuri kwa mashindano haya makubwa, hatuendi tu kushiriki bali tunataka kushindana na kufanya vizuri,” amesema Mangula.
Mashindano ya Chess Olympiad ni miongoni mwa matukio makubwa zaidi katika mchezo wa chess duniani, yakihusisha timu za taifa kutoka nchi nyingi zinazokwenda kuonesha uwezo wao katika mashindano ya kiwango cha juu.




