LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo mitatu kupigwa Dar es Salaam, Morogoro na Kagera.
Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa Ihefu kwenye uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya Dar es salaam.
Ihefu na Ruvu Shooting zina pointi 11 kila moja baada ya michezo 15 lakini Ihefu ipo nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi huku Ruvu ikishika nafasi ya 15 kutokana na tofauti ya mabao.
Mkoani Morogoro, Namungo ni mgeni wa Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Manungu uliopo Turiani.
Mtibwa Sugar inashika nafasi ya 6 ikiwa na pointi 22 baada ya michezo 15 wakati Namungo ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 18 baada ya michezo 15 pia.
Katika mchezo mwingine Kagera Sugar itaikaribisha Azam kwenye uwanja wa Kaitaba uliopo Bukoba, Kagera.
Azam ipo nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 25 baada ya michezo 15 wakati Kagera Sugar ipo nafasi ya 7 ikiwa na pointi 21 baada ya michezo 15
Katika mchezo mmoja wa ligi uliopigwa Desemba 15 uwanja wa Uhuru Dar es salaam wenyeji KMC imeutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kuifunga Coasta Union bao 1-0.




