Vipimo vya afya vyamliza Dipika Kakar

MUMBAI: Muigizaji wa India Dipika Kakar ameshindwa kuzuia hisia zake alipomwaga machozi wakati mumewe Shoaib Ibrahim alipokumbusha kuhusu vipimo vipya vya damu atakavyofanyiwa baada ya sikukuu ya Eid.
Katika video mpya waliyochapisha kwenye YouTube, Shoaib alieleza kuwa Dipika amekuwa akifuata ratiba maalum ya lishe na mazoezi, ikiwemo kuamka mapema asubuhi kwa ajili ya matembezi na kuepuka kula baada ya saa moja jioni.
Hata hivyo, alipotaja kuwa baada ya wiki nne mkewe atalazimika kufanya vipimo vya damu, Dipika alionekana kuguswa sana kihisia na kufuta machozi.
Muigizaji huyo amesema tangu alipofanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ini kufuatia saratani ya hatua ya pili, bado ana hofu juu ya hali yake ya afya, ingawa anaendelea kuwa na matumaini.
Dipika amekuwa akishirikisha mashabiki wake hatua kwa hatua kuhusu safari yake ya matibabu kupitia vlog zake za YouTube.




