Umuhimu wa Raphinha Barcelona haupimiki

JEDDAH:KAMA bado kulikuwa na mtu anajiuliza Raphinha ana umuhimu gani ndani ya Barcelona, basi majibu yako wazi kabisa. Tangu arejee kwenye kikosi cha kwanza baada ya kupona maumivu ya misuli ya paja, Barca imegeuka mashine ya ushindi, ikipeleka kibindoni mechi zote wanazocheza.
Takwimu zinasema kila kitu. Barcelona imeshinda mechi zote 10 mfululizo tangu Raphinha aliporudi kwenye kikosi cha kwanza baada ya kupona jeraha la ‘hamstring’. Hakuna sare, hakuna kipigo. Mechi 10, wameshinda 10. Hapo ndipo unapoanza kuelewa uzito wa huyu Mbrazil ndani ya timu ya Hansi Flick.
Kurejea kwake kumeipa Barcelona kasi mpya, njaa mpya na ubunifu mkubwa zaidi mbele. Upande wake umekuwa tishio muda wote, akichangia mabao, pasi za mwisho na kuisukuma timu kucheza kwa kujiamini zaidi. Sio tu anafunga au anatengeneza, bali anaipa timu roho na ushindani.Si uliona namna alivyojaribu kuokoa bao lile ambalo badae likaja kufungwa na Gonzalo Garcia?
Kwa mwenendo huu, siyo ajabu kuona mashabiki na wachambuzi wakisema wazi kuwa Raphinha kwa sasa ni mmoja wa wachezaji muhimu zaidi ndani ya kikosi cha Barcelona. Na matokeo haya 10 mfululizo yanaonesha hilo bila hata kutia chumvi nyingi.




