Serie A

Ulaya ukizingua tu kibarua huna!

MILAN:AC Milan wametangaza rasmi kumfuta kazi Paulo Fonseca kama kocha mkuu wa timu ya wanaume kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Roma.

Katika taarifa rasmi, klabu ilisema: “AC Milan inatangaza kuwa Paulo Fonseca ameachishwa majukumu yake kama Kocha Mkuu wa Timu ya Kwanza ya Wanaume. Klabu inatoa shukrani zake kwa taaluma yake kubwa na inamtakia mafanikio mema katika siku zijazo.”

Fonseca mwenyewe alithibitisha kuachishwa kwake alipokuwa akiondoka uwanjani kwa gari baada ya mechi hiyo. “Ndiyo, ni kweli, nimetimuliwa Milan. Hivi ndivyo maisha yalivyo. Ninatambua nilifanya kila nilichoweza,” alisema. Hata hivyo, kulingana na ripoti za Sky Sport, uongozi wa Milan ulikuwa ukifikiria uamuzi huu kwa muda mrefu kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Fonseca alikumbwa na changamoto za matokeo duni pamoja na migogoro na wachezaji nyota kama Leao, Theo Hernandez, na Calabria. Timu kwa sasa ipo nafasi ya nane kwenye Serie A ikiwa na pointi 27, ikiachwa pointi 14 nyuma ya vinara na pointi 8 nje ya nafasi za Ligi ya Mabingwa.

Sergio Conceicao, raia mwenzake wa Ureno, anatarajiwa kuchukua nafasi hiyo. Kocha huyo mpya ataongoza mechi yake ya kwanza katika nusu fainali ya Super Cup dhidi ya Juventus Januari 3.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button