UCL yaanza ‘mbilinge’ kuelekea Mei 30

MONACO: SAFARI ya kipute cha ligi ya mabingwa barani ulaya (UCL) imeanza rasmi baada ya mechi za ligi hiyo kuwekwa hadarani baadae Agosti 28. Mabingwa Paris St Germain watavaana na Bayern Munich na Barcelona huku washindi mara 15 Real Madrid wakimenyana na Manchester City na Liverpool.
PSG pia itakutana na timu za Premier League Tottenham Hotspur na Newcastle United pamoja na Atalanta na Bayer Leverkusen katika mfumo mpya wa jedwali ulioanza msimu uliopita ambapo kila klabu inacheza michezo nane, minne nyumbani na minne ugenini.
Real Madrid itacheza tena na Manchester City kwa msimu wa tano mfululizo kisha kuwa na safari ya kuelekea Liverpool katika mechi ambayo itamrudisha beki Trent Alexander-Arnold nyumbani baada ya kutimkia madrid mwishoni mwa msimu uliopita. Los Blancos pia watavaana na Juventus Pamoja na wageni wa michuano hiyo Kairat Almaty ya Kazakhstan.
Wababe wengine wa England Manchester City na meneja wao Pep Guardiola watamribisha kiungo wao mwenye historia kubwa Kevin De Bruine anayerejea Etihad na klabu yake mpya ya Napoli kisha kuvaana pia na Dortmund, Bayer Leverkusen na timu za LaLiga Real Madrid na Villarreal
Vinara wa ligi hiyo msimu uliopita Liverpool pia watakwaa kisiki cha mshindi wa pili wa msimu uliopita Inter Milan, kabla ya kukutana Atletico Madrid na Eintracht Frankfurt, huku Bayern wakicheza na Chelsea, Arsenal na Club Brugge.
Washindi wa pili wa msimu uliopita Inter Milan watawakaribisha Liverpool na Arsenal, na timu hiyo ya Italia itasafiri kuwafuata Borussia Dortmund na kumaliza na Atletico Madrid.
Barcelona, mabingwa wa LaLiga na wana-nusu fainali wa msimu uliopita watawakaribisha PSG na watakutana na mechi za ugenini dhidi ya Chelsea na Newcastle.
Arsenal, waliotinga nusu fainali msimu uliopita, pia wanacheza na Atletico Madrid na Club Brugge huku wakitarajia kukutana na wapinzani wao wakubwa Bayern Minich, ambao wamekutana nao mara 14 kwenye michuano hiyo, na wameshindwa kuwafunga katika mechi tano zilizopita wakipokea idadi ya jumla ya mabao 18 na wakiwafunga matano.