Africa

Twiga Stars waanza maandalizi ya Wafcon

DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, imeanza rasmi mazoezi katika Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Kigamboni, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 zitakazofanyika nchini Morocco.

Tanzania imepangwa Kundi B la mashindano hayo pamoja na mabingwa watetezi Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso, katika kundi linalotarajiwa kuwa na ushindani mkali.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Machi 17 mwaka huu, ambapo Twiga Stars itaanza kampeni yake siku hiyo hiyo kwa kuwakabili Afrika Kusini katika Uwanja wa Al Medina, Rabat.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime, tayari aliwaita jumla ya wachezaji 30 kwa ajili ya kambi ya maandalizi, kikosi ambacho kimejumuisha mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu wa kimataifa, chipukizi pamoja na wakongwe, lengo likiwa ni kujenga timu imara na yenye ushindani mkubwa.

TFF imeeleza kuwa maandalizi ya mapema ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha Twiga Stars inafanya vizuri katika mashindano hayo makubwa ya bara, huku matarajio yakiwa ni kuona timu hiyo ikiweka historia mpya katika WAFCON 2026.

Related Articles

Back to top button