Twende kilioni: Nywele za mkono sasa ofisini na kila kona

KARIBU kwa mara nyingine upate ladha ya mitindo na mvuto wa kipekee, na leo ukurasa wetu wa urembo na mitindo unakuletea mwelekeo unaoendelea kuitikisa jamii kwa kasi kubwa, usukaji wa nywele za mkono maarufu kama Twende Kilioni, sambamba na mitindo ya kuchora maumbo, mistari na hata maneno kichwani.

Zamani watu walizoea kuona nywele za mkono kama mitindo ya mitaani au ya ndani tu, lakini leo hali imebadilika kabisa. Twende Kilioni sasa ni staili rasmi. Unaziona ofisini, kanisani, msikitini, kwenye harusi, sherehe kubwa na hata kwenye majukwaa ya heshima, bungeni na kwenye taasisi za juu kabisa.
Usukaji wa nywele za mkono si suala la kupendeza tu, ni sanaa. Kila muundo una ujumbe wake. Kuna wanaochora mistari, maumbo ya kipekee, alama, kopa au hata maneno. Yote haya yanamfanya mtu aonekane wa kisasa, mbunifu na mwenye kujiamini. Ndio maana mitindo kama twende kilioni, Kilimanjaro, jicho la samaki, jicho la mke mwenza, zigizaga na mingine mingi inaendelea kuzaliwa kila siku kulingana na ubunifu wa msusi na ladha ya mteja.

Kilichoongeza nguvu ya mtindo huu ni jinsi ulivyoingia rasmi kwenye maisha ya kila siku. Wasichana, wanawake na watoto wamekuwa mstari wa mbele kusuka staili hii kwa sababu ni rahisi, hazina usumbufu na zinaonesha uhalisia wa mtu. Tofauti na zamani, leo mtu anaweza kwenda kazini, kwenye ibada au kwenye kikao muhimu akiwa na nywele za mkono bila kuonekana kama yuko nje ya mstari.
Uzuri mwingine wa nywele za mkono ni kwamba zinaenda na kila aina ya mavazi. Uvae suti, tisheti na jeans, gauni au hata habaya, bado staili inakaa sawa. Pia ni rafiki sana kipindi cha joto kwa sababu ni nyepesi na rahisi kutunza. Kwa upande wa gharama, si nzito. Bei nyingi zinaanzia Sh 1,000 kwenda juu kulingana na mtindo, na kwa macho ya watu, mtu anayesuka nywele za mkono mara nyingi huonekana nadhifu na mrembo.
Cha kuvutia zaidi, nywele za mkono hazichagui. Haziangalii rangi, umbo la mwili wala umri. Uwe mnene au mwembamba, mrefu au mfupi, kila mtu anaweza kusuka na akaonekana freshi, wa kisasa na anayejijali.
Ingawa usukaji wa nywele umetokana zaidi na utamaduni wa Afrika, leo umevuka mipaka. Mataifa mbalimbali duniani yameanza kuukumbatia mtindo huu, jambo lililobadili kabisa mtazamo wa zamani kuhusu nywele za asili za Mwafrika. Wasanii na watu maarufu wamekuwa mabalozi wakubwa wa mabadiliko haya, wakionesha hadharani mitindo yao na kuwafanya watu wengi zaidi kuanza kujiamini.

Kitaalamu pia, kusuka nywele za mkono bila rasta husaidia kulinda ngozi ya kichwa, kurahisisha uotaji wa nywele na kukuonesha sura yako halisi bila kujificha nyuma ya mitindo mizito.
Mwisho wa siku, Twende Kilioni si staili tu, ni utambulisho. Ni njia ya kujiambia na kuwaambia wengine kuwa unajipenda, unajiamini na unaenda na wakati. Kwa sababu urembo si anasa, ni sehemu ya wewe.




