Filamu

Tuzo za Tamasha la Filamu Tanzania kufanyika Februari 14

DAR ES SALAAM:TUZO za Tamasha la Filamu Tanzania (Tanzania Film Festival Awards) zinatarajiwa kufanyika Februari 14, 2016 katika ukumbi wa The Super Dome, uliopo Masaki jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kutangaza vipengele vya tuzo hizo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Gervas Kasiga, alisema kuwa tuzo hizo zinatarajiwa kuacha alama kubwa katika sekta ya filamu nchini kutokana na wingi na ubora wa kazi zilizowasilishwa.

Kasiga amesema kuwa zaidi ya kazi 2,000 za filamu kutoka Tanzania zilikusanywa na kuchujwa hadi kubaki kazi 200 bora, huku kazi za nje ya nchi zikiwa zaidi ya 200, jambo linaloonesha ukubwa wa tamasha hilo kimataifa.

“Ninawakaribisha wasanii na wadau wote wa filamu kujitokeza kwa wingi siku ya wapendanao ili tufurahie na kupokea tuzo zetu. Waswahili ni watu wa kipekee wenye upekee wao,” amesema Kasiga.

Kwa upande wake, Sophia Mgaza, akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa usiku wa tuzo hizo utapambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa Tanzania, Kenya na Uganda.

Ameongeza kuwa tamasha hilo limewakutanisha wasanii kutoka nchi zaidi ya tisa.Tamasha hilo lina vipengele 26 vya tuzo, vikiwemo Mwigizaji Bora wa Kike na Kiume, Mwigizaji Chipukizi Bora wa Kike na Kiume pamoja na vipengele vingine muhimu vinavyolenga kukuza vipaji vya filamu.

Naye Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Rajab Amir, ameishukuru Bodi ya Filamu na wadau wote kwa mchango wao mkubwa katika kukuza sekta ya filamu nchini kwa kutambua na kuthamini kazi za waigizaji.

Hata hivyo, ameiomba serikali kuunga mkono tuzo hizo kwa kutoa tuzo zenye bahasha ili kuwapa wasanii hamasa zaidi na kuwafanya wajivunie mafanikio yao kama alama ya thamani katika kazi zao za sanaa.

Related Articles

Back to top button