Africa

Tuzo za CAF: Hakimi mchezaji bora Afrika, Morocco yang’aa

RABAT: NAHODHA wa timu ya taifa ya Morocco, Achraf Hakimi, ameibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa upande wa wanaume katika tuzo za CAF zilizofanyika usiku wa jana Jumatano, akihitimisha msimu ambao alinyanyua taji la UEFA Champions League na klabu yake ya Paris Saint-Germain (PSG).

Beki huyo wa kulia mwenye umri wa miaka 27 pia alitwaa ubingwa wa Ligue 1 kwa mara ya nne mfululizo msimu uliopita, pamoja na Kombe la Ufaransa na UEFA Super Cup. Hata hivyo, PSG walishindwa kutwaa Kombe la Dunia la Klabu, ambapo Hakimi alilazimika kutosheka na medali ya mshindi wa pili jijini New York.

Hakimi aliwashinda washindi wa zamani Mohamed Salah wa Liverpool na Victor Osimhen wa Galatasaray, na kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza katika safari yake ya soka.


“Ni heshima kubwa kuwa hapa leo. Najivunia kushinda tuzo hii muhimu,” alisema Hakimi huku akiwashukuru familia yake, wachezaji wenzake na kocha wa Morocco, Walid Regragui.

Kwa sasa, Hakimi anaendelea kuuguza majeraha ya kifundo cha mguu, lakini iwapo atapona kwa wakati anatarajiwa kuwaongoza wenyeji Morocco kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kuanzia Desemba 21, wakisaka taji lao la kwanza tangu mwaka 1976.

Morocco pia ilitawala upande wa wanawake, baada ya Ghizlane Chebbak kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika, akiwashinda Mtunisia Sanaa Mssoudy na nyota wa Nigeria, Rasheedat Ajibade. Chebbak, anayekipiga Al Hilal, alikuwa mfungaji bora wa michuano ya Afrika kwa wanawake mwaka huu licha ya timu yake kupoteza dhidi ya Nigeria katika fainali.

Ilikuwa siku yenye mafanikio makubwa kwa taifa hilo lililoandaa sherehe hizo, baada ya Yassine Bounou kutwaa tuzo ya Kipa Bora wa Afrika kwa upande wa wanaume, huku timu ya taifa ya Morocco ya chini ya miaka 20 mabingwa wa Kombe la Dunia ikitangazwa kuwa timu bora ya taifa kwa upande wa wanaume.

Othmane Maamma wa Watford mwenye umri wa miaka 20 alishinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi kwa upande wa wanaume, huku Doha El Madani akitetea taji lake kama Mchezaji Chipukizi Bora wa upande wa wanawake.

Kocha wa Cape Verde, Bubista, alinyakua tuzo ya Kocha Bora wa mwaka kwa upande wa wanaume baada ya kuipeleka nchi yenye watu takribani 525,000 katika fainali za Kombe la Dunia 2026.

Kwa upande wa wanawake, kipa wa Nigeria Chiamaka Nnadozie aliweka historia kwa kushinda tuzo ya Kipa Bora wa Afrika kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Related Articles

Back to top button