“Tunaendelea kumtathmini Rodri” – Toure

MANCHESTER: MANCHESTER City wataendelea kummkosa kiungo wao muhimu, Rodrigo Hernandez Cascante maarufu ‘Rodri’, katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace Jumapili, huku mshindi huyo wa Ballon d’Or akiendelea kuimarika baada ya majeraha ya nyama za misuli ya paja yaliyomweka nje tangu Oktoba.
Man City wangependa kumrejesha uwanjani kiungo huyo raia wa Hispania mwenye umri wa miaka 29 katika mbio zao za ubingwa, hasa baada ya kupunguza pengo la pointi na Arsenal na sasa kukaa pointi mbili tu nyuma ya vinara hao baada ya mechi 15.
“Rodri anafanya mazoezi vizuri sana. Anaonekana kuwa fiti zaidi kila siku, lakini nina uhakika hatutamwona wikendi hii. Anaendelea vizuri kwenye hatua za kurejesha ubora wake.” – amesema kocha msaidizi wa klabu hiyo, Kolo Toure.

Toure amezungumza kwa niaba ya kocha mkuu Pep Guardiola, ambaye hakufika kwenye mkutano na waandishi wa habari kutokana na sababu binafsi ambazo klabu imethibitisha kuwa hazitaathiri uwepo wake Jumapili.
Kwa upande mwingine, beki John Stones, ambaye alikosekana kwenye ushindi wa 2-1 dhidi ya Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Jumatano na pia hakushiriki ushindi wa 3-0 dhidi ya Sunderland wiki iliyopita, bado anafanyiwa tathmini.
Toure pia amethibitisha kuwa mchezo wa Jumapili utakuwa wa mwisho kwa Omar Marmoush na Rayan Ait-Nouri kabla ya kuondoka kujiunga na timu zao za taifa Misri na Algeria kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, zinazoanza Desemba 21.




