Ten Hag atua Leverkusen

LEVERKUSEN:BAADA ya kuondoka Manchester United Oktoba 2024, Erik ten Hag sasa anarejea Bundesliga kuchukua mikoba ya Xabi Alonso katika klabu ya Bayer Leverkusen, mabingwa wa Bundesliga na DFB Pokal msimu wa 2023/24.
Kocha huyo raia wa Uholanzi (miaka 55), ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili(hadi 2027) kuanzia Julai 1, amesema:
“Leverkusen ni miongoni mwa klabu bora Ujerumani na Ulaya. Nipo hapa kuendeleza mafanikio na kujenga kikosi cha ushindani katika kipindi hiki cha mpito.”
Ten Hag anakuja na uzoefu mkubwa, akiwahi kung’ara Ajax kwa mataji matatu ya Eredivisie na kufika nusu fainali ya UEFA Champions League 2019. Pia alishinda EFL Cup na FA Cup akiwa na Manchester United.
Mechi yake ya kwanza rasmi na Leverkusen itakuwa raundi ya kwanza ya DFB Pokal kati ya Agosti 15–18, kabla ya kuanza msimu mpya wa Bundesliga.
Je, Ten Hag ataendeleza moto ulioachwa na Alonso?