Tanzania yatingisha mashindano ya Motokrosi Afrika ya Kati

KAMPALA:TIMU ya Taifa ya mchezo wa mbio za pikipiki kutoka Tanzania imeibuka na mafanikio makubwa baada ya kuiwakilisha nchi kwa kishindo katika mashindano ya Ubingwa wa Motokrosi Afrika ya Kati yaliyofanyika nchini Uganda, na kumalizika Aprili 21.
Katika mashindano hayo yaliyowakutanisha madereva bingwa kutoka mataifa mbalimbali, Tanzania iliwakilishwa na madereva waliotia fora katika makundi mawili tofauti: Daraja la Kawaida (MX2) na Daraja la Juu (MX1).
Katika kundi la MX2, ambalo linahusisha pikipiki zenye injini ndogo (kawaida 250cc 4-stroke) na huwashirikisha madereva chipukizi au wanaoanza taaluma ya kitaalamu, Mtanzania Juma Khalef aliibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza, na kuiwezesha Tanzania kujizolea heshima kubwa.
Kwa upande wa MX1, maarufu kama Premium Class, Tanzania ilionesha uwezo wa hali ya juu pia. Katika kundi hili linalohusisha pikipiki zenye injini kubwa (hadi 450cc kwa 4-stroke), Masoud Seif alishika nafasi ya pili huku Kelvin Okyo akifuata kwa nafasi ya tatu. Nafasi ya kwanza katika daraja hili ilinyakuliwa na dereva mwenyeji kutoka Uganda.

Mbio za pikipiki aina ya Motokrosi (Motocross) ni mchezo unaofanyika katika mazingira yenye changamoto kama milima, mbuga, au uwanja wa mchanga wenye vizingiti vya kuruka, kona ngumu, na maeneo yenye kupima ujuzi wa mpanda pikipiki.
Katika makundi ya MX1 na MX2, kiwango cha injini pamoja na uzoefu wa dereva ndicho kinachoamua mahali pa kushiriki.
Kwa mafanikio haya, Tanzania imeendelea kudhihirisha kuwa ina vipaji na uwezo mkubwa kwenye mchezo huu wa kasi na ujasiri, huku wakiwa wameipeperusha vyema bendera ya taifa katika anga za kimataifa.




