Tamasha la ZIFF lazinduliwa kwa maandamano

ZANZIBAR:TAMASHA la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) limezinduliwa rasmi kwa maandamano ya shamra shamra yaliyofanyika asubuhi ya leo 25, 2025 licha ya kuwepo kwa mvua kubwa.
Maandamano hayo ya amani ya kilomita tano yaliyoongozwa na Bendi ya Jeshi la Polisi yalianzia Forodhani yakapitia Darajani, Maisara, Vuga, na yakaishia Ngome Kongwe maeneo ya Forodhani.
Maandamano haya, yaliyowaleta pamoja maelfu ya wakazi wa Zanzibar na wadau wa filamu, yalitawaliwa na shangwe na vifijo.
Mratibu wa Jukwaa la wanawake na Vijijini la ZIFF Sabrina Faraja amesema kwamba: “Maandamano haya ni kitu cha maana sana kila mwaka ZIFF inapoanza huwa na maandamano kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Tamasha hilo.”
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe, ambaye ndiye mwenyeji wa Tamasha hilo, Mhandisi Ali Said Bakar, amesisitiza umuhimu wa ZIFF kwa jamii,
Katika hotuba hiyo iliyosomwa kwa Niaba yake na Ofisa kutoka Mamlaka hiyo Asha Ali Hassan amesema kwamba tamasha hilo likitimiza miaka 28 limeonesha kuwa msaada mkubwa kwa jamii na katika uchumi wa Zanzibar ikiwamo kutunza utamaduni na sanaa ya filamu.
Aidha Mhandisi Bakar alisisitiza umuhimu wa mazoezi ya kimwili na kiakili, akisema, “Hapa leo tunaungana kwa kufanya mazoezi, kwani ni moja kati ya tiba ya kimwili na akili katika ufanisi wa kazi zetu za kila siku.”
Tamasha hilo lenye kauli mbiu ya ‘TUMAINI LINAPOCHIPUKIA linatarajiwa kukamilika Juni 29 mwaka 2025 kwa kutoa tuzo kwa washiundi mbalimbali watakaoshinda kupitia vipengere kadhaa vya ubora wa filamu walizoziwasilisha.