Special Olympics yawafunda wanahabari za michezo

DAR ES SALAAM: SPECIAL Olympics Tanzania imeendesha mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari za michezo kutoka vyombo mbalimbali nchini, yakilenga kuongeza uelewa kuhusu namna bora ya kuripoti na kuhabarisha jamii juu ya vipaji vya watu wenye ulemavu wa akili kupitia michezo.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Benjamin William Mkapa Dar es Salaam jana yamekusudia kujenga ushirikiano imara kati ya vyombo vya habari na Special Olympics Tanzania, ili kuhakikisha simulizi chanya kuhusu uwezo na mafanikio ya watu wenye ulemavu wa akili zinapata nafasi kubwa zaidi katika vyombo vya habari.
Mafunzo haya ni sehemu ya mpango endelevu wa Special Olympics Tanzania wa kuimarisha ushirikiano na wadau wa habari ili kuendeleza ajenda ya ujumuishaji na fursa sawa katika sekta ya michezo kwa watu wote.
Makamu Mwenyekiti wa Special Olympics Tanzania, Muharami Mchume, amesema semina iliyotolewa kwa waandishi wa habari imelenga kuwawezesha kuelewa kwa undani zaidi shughuli na falsafa ya Special Olympics nchini.
Akizungumza wakati wa kufunga semina hiyo, Mchume alisema taasisi hiyo inaamini vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kukuza michezo kwa wanariadha wenye ulemavu wa akili, sambamba na kupambana na unyanyapaa dhidi yao.

“Kupitia kampeni ya kimataifa ya ushirikishwaji , tunataka kuona watoto hawa wakishirikishwa na wenzao katika michezo na jamii kwa ujumla. Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kusaidia kuonesha kuwa nao wana uwezo na wanapaswa kupata nafasi sawa,” alisema Mchume.
Amina Kasheba, mmoja wa washiriki wa semina hiyo, alisema amepata maarifa mapya yatakayomsaidia kuripoti habari za michezo kwa usahihi na ubunifu zaidi.
“Semina hii imenifungua macho. Nitajitahidi kuwa mstari wa mbele kuandika habari kuhusu wanariadha wa Special Olympics Tanzania na kuzitangaza kwa wigo mpana zaidi,” alisema Amina.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Special Olympics Tanzania, Charles Rays, alisema taasisi hiyo inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kukuza michezo kwa watu wenye ulemavu wa akili na itaendelea kushirikiana nao kwa karibu.
“Vyombo vya habari ni wadau muhimu. Tukifanya kazi pamoja, tunaweza kubadilisha mitazamo ya jamii na kuongeza ushiriki wa wanariadha wetu katika mashindano mbalimbali,” alisema




