Soka Ufukweni kulisaka Kombe la Dunia

Timu ya Taifa ya soka la Ufukweni imedhamiria kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye michezo ya pili ya soka la ufukweni Afrika itakayofanyika Tunisia baadae mwezi huu.

Akizungumza leo Dar es Salaam Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Henry Tandau amesema wanaamini kutakuwa na uwakilishi mzuri wa timu ya Tanzania kwenye michuano hiyo ya Ufukweni huku akiweka bayana sababu ya Tanzania kualikwa kushiriki michuano hiyo ya Afrika.
“Imeonekana timu yetu ya soka la Ufukweni ipo nafasi ya nane kwenye viwango vya ubora Afrika, hivyo tukafuzu kushiriki michuano hiyo, licha ya kwamba tumepata taarifa kwa kuchelewa lakini tutashiriki na tunaamini tutafanya vizuri,”amesema Tandau.
Mkuu wa Msafara wa timu ya Tanzania itakayokwenda Tunisia Suleiman Ame amesema anaamini hakuna kitakachowakwamisha kuelekea michuano hiyo.
“Maandalizi yatafanyika vizuri, maandalizi ya awali tayari yamekwisha fanywa na kamati ya Olimpiki na tunaamini yataendelea kufanyika, Mungu akitujalia naamini tutaipa nchi heshima” Amesema Ame.
Kwa upande wake kocha wa timu hiyo Boniface Pawasa amesema atawaandaa vijana wake ili kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na wataitumia kama fursa kwao.
” Tumelipokea hili vizuri sana na tunatamani kuyatumia mashindano haya ili kujitangaza mimi kama kocha na hata wachezaji, tunatamani sana kushiriki michuano ya Kombe la Dunia,” amesema Pawasa.
Iwapo timu hiyo ya Tanzania itapata nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo ya pili ya Afrika, itafuzu kucheza Fainali za Kombe la dunia kwa soka la Ufukweni zitakazofanyika Indonesia kuanzia Agosti mwaka huu.