
MSANII mkongwe katika muziki wa hip hop nchini, Issa Iddy maarufu Slota kutoka kundi la LWP Majitu ameweka wazi kwamba wasanii wengi wa bongo fleva hawaalikwi katika matamasha makubwa ya muziki ndani na nje ya nchi kwa sababu hawana uwezo wa kuimba live na bendi.
Slota amesema wasanii wa sasa hawana pumzi ya kuimba live kwa saa kadhaa jukwaani ndiyo maana mialiko katika matamasha makubwa ya muziki hawapati badala yake wanaalikwa wasanii wa muziki wa dansi na wasanii wa muziki wa asili.
“Wasanii wa muziki wa kizazi kipya wa miaka ya 80 wengi wao tulikiwa na uwezo wa kuimba live na wengi wetu tumeshaimba katika matamasha makubwa duniani lakini wasanii wa sasa bado wanachangamoto kubwa ya kuimba live hawana pumzi na muziki wa kwenye matamasha makubwa unataka muziki live ndiyo maana wasanii wengi wa bongo hawaalikwi.
Hata tamasha kubwa la muziki linalofanyikaga Zanzibar kila mwaka nalo ukichunguza wasanii wanaoalikwa wengi wao ni wanaoimba na bendi lakini hawa mmoja mmoja hawapati mialiko,” amesema Slota.
Slota na kundi lake la LWP Majitu walijipatia umaarufu kupitia wimbo wa ‘Jela’ na ‘Mke wa Mtu Sumu’ amesema muziki wa sasa umefika kimataifa hivyo hautaki ‘Play back’ mashabiki wanaohudhuria matamasha hayo wanahitaji kusikia vyombo vikipigwa live na wasanii wakiimba live.
“Muziki una njia zake na muziki wa matamashani unataka kila kitu kionekane kama hauna pumzi utajulikana tu na watu watakupigia kelele za kukuaibisha ila kama unauwezo wa kuimba live utafurahia zaidi muziki na utakuwa na wigo mpana wa kufanya biashara ya muziki katika mataifa mbalimbal” amemaliza Slota ‘Kuku kwa Mrija’ na ‘Raha’.




