Africa

Singida Black Stars waahidi ushindani Kigali

KIGALI: SINGIDA Black Stars imewasili salama jijini Kigali, Rwanda, tayari kwa mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Rayon Sports utakaochezwa kesho ijumaa huku wakiahidi kufanya vizuri.

Akizungumza baada ya kuwasili, Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza alisema kikosi kipo tayari kwa mtanange huo na kwamba wachezaji wapo kwenye hali nzuri ya kisaikolojia na kiafya.

“Hautakuwa mchezo mwepesi kwa sababu Rayon ni timu nzuri na imekuwa ikifanya vizuri. Morali tuliyonayo baada ya kutwaa ubingwa wa CECAFA Kagame Cup imeongeza ari na kujiamini ndani ya kikosi chetu. Pamoja na hayo, bado tunamheshimu mpinzani,” alisema Masanza.

Singida chini ya Kocha Mkuu wa zamani Miguel Gamondi imetoka kuchukua ubingwa wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) baada ya kuifunga timu ya Sudan Al Hilal mabao 2-1 katika mchezo wa fainali.

Masanza aliongeza kuwa mashabiki watarajie kuona mchezo wenye ushindani mkubwa, kwani dhamira ya timu ni kupambana kuhakikisha wanapata matokeo chanya ugenini.

Kikosi cha wachezaji 26 kimeambatana na benchi la ufundi nchini Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

Related Articles

Back to top button