Mapinduzi CupNyumbani

Simba, Yanga, Azam kunogesha Mapinduzi

MSIMU wa 17 wa fainali za Kombe la Mapinduzi unatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari Mosi hadi 13, 2023 katika Uwanja wa Amaan Visiwani Zanzibar.

Jumla ya timu 12 zitashiriki fainali za mwaka huu zikiwa zimepangwa katika makundi manne ambapo mpaka sasa msisimko unaonekana kuwa mkubwa kutokana na maandalizi
yaliyofanywa na waandaji pamoja na ubora wa timu zitakazoshiriki.

Mabingwa watetezi wa taji hilo Simba, wamepangwa Kundi C pamoja na wenyeji Mlandege na KVZ wakati miamba ya soka Tanzania Bara, Yanga wenyewe wamepangwa Kundi B,
pamoja na Singida Big Stars na Mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar KMKM.

Kundi A linaundwa na washindi wa pili wa msimu uliopita Azam FC, wenyeji Mlandege na Jamhuri ya Pemba na Kundi D litawakilishwa na timu za Namungo, Aigle Noir ya Burundi na Chipukizi ya Pemba.

Mabingwa watetezi Simba watafungua dimba Januari 3 kwa kucheza na Mlandege mchezo ambao unatarajiwa kuanza saa 2: 15 baada ya mchezo wa mapema kati ya Azam FC na Malindi.

Simba ambayo inashikilia rekodi ya kubeba Kombe la Mapinduzi mara nyingi, msimu huu italazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inalitetea taji hilo vinginevyo mambo yanaweza kuwa magumu kutokana na ubora wa timu zinazoshiriki.

Uhakika wa kuvuka kwenye mechi za hatua ya makundi ni mkubwa lakini kutoka hapo kwenda nusu fainali na fainali kuna kazi kubwa hkama atakutana na watani zao Yanga, Singida Big Stars, Azam FC au Eangle Noir timu ambazo zinaweza kuisumbua.

Hiyo inatokana na mapungufu iliyoyaonesha kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, ingawa kwa sasa uongozi wa timu hiyo upo kwenye mchakato wa kukiboresha kikosi hicho
kwa kufanya usajili baada ya kumwongeza mkongwe Saido Ntibazonkiza kutoka Geita Gold.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi ndio anatarajia kuzindua mashindano hayo huku bingwa wa mwaka huu akitarajiwa kuondoka na fedha taslimu Sh milioni 23 hiyo ikiwa ni tofauti na miaka iliyopita ambapo bingwa alikuwa akiondoka na Sh milioni 10.

Mashindano hayo yana historia ndefu, licha ya kuchukuliwa kisiasa zaidi, lakini ukweli ni moja ya michuano iliyojipatia umaarufu na imekuwa ikiwapa burudani wakazi wa visiwani
wenye mapenzi na mchezo wa soka.

Tangu kuasisiwa kwa mashindano hayo mwaka 2007, vipaji vingi vimeibuka na kuwa msaada mkubwa kwa timu za taifa za Tanzania na ile ya Zanzibar Heroes ingawa timu wenyeji kutoka Zanzibar zimekuwa wasindikizaji tu.

Rekodi za michuano hiyo ambayo awali ilishirikisha timu za visiwani pekee miaka ya 2000 kabla ya kubadilishwa mwaka 2007 na kuchezwa katika mfumo wa sasa wa kushirikisha
timu za Bara na nyingine kutoka nje ya Tanzania ingawa kwa sasa utamaduni wa kuzialika timu kutoka nje uliachwa takribani misimu mitatu iliyopita.

Mbali na mashindano hayo kuadhimisha mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12 na kuibua vipaji vya soka lakini mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza vipaji vya soka Tanzania nzima.

Kombe la Mapinduzi lina maana kubwa kwa soka la Zanzibar ambalo Ligi Kuu yake ipo chini na ina idadi ndogo ya timu zinazoshiriki hivyo kwa msimu mzima wachezaji wanacheza
mechi chache ambazo zinawafanya kutokuwa fiti.

Faida nyingine inayopatikana kwenye mashindano hayo ni baadhi ya wachezaji waliong’ara kusajiliwa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, na kupata ushindani wa kweli
kutokana na ugumu ligi yenyewe.

Tangu kufutwa kwa Ligi ya Muungano, timu za Zanzibar zimekuwa hazipati changamoto na wapo wanaoamini kuwa hiyo ni sababu ya timu hizo kutolewa mapema kwenye Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ni dhahiri katika mazingira ya aina hiyo, michuano ya Kombe la Mapinduzi inaweza kuwa na maana kubwa katika soka la Tanzania kwa ujumla Kwa timu za Tanzania Bara ukiacha
kuonesha ubora na mabavu yao dhidi ya timu za Zanzibar lakini kwa mwaka huu klabu za Simba na Yanga zitatumia mashindano hayo kama maandalizi kuelekea mechi za hatua
ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ubora wa timu ambazo zimepangwa kundi moja na klabu za Simba na Yanga na kama zitafanikiwa kuendelea hatua ya robo fainali na fainali niwazi itakuwa maandalizi tosha kwao kuelekea kuanza kwa mechi hizo za makundi Febuari.

Hapana shaka mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa mwaka huu timu za Zanzibar zitakuwa zimepata dawa ya kutibu maradhi yanayowafanya watolewe mapema na kuwaacha wageni.

Timu kama KMKM, Mlandege, KVZ zinaweza kufanya makubwa na kuwashangaza wengi kutokana na maandalizi waliyofanya kuelekea kwenye mashindano ya mwaka huu.

Kufanya vizuri kwa timu wenyeji kutamaliza ufalme wa Simba na Yanga ambazo ndio timu pekee ambazo zimekuwa zikikusanya idadi kubwa ya watazamaji kwenye mashindano hayo
kutokana na timu wenyeji kutolewa mapema.

Related Articles

Back to top button