Nyumbani

Simba yafungua ukurasa mpya

Yaoga mabilioni, yatupa jiwe gizani

DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba imeingia kwenye ukurasa mpya wa maendeleo baada ya kuitangaza rasmi kampuni ya Jayrutty Investment Company kuwa mzabuni mpya wa kusambaza vifaa na bidhaa za klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Shilingi bilioni 38.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza zabuni hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uzabuni ya Simba, Seif Muba, amesema kuwa baada ya kupokea maombi mengi kutoka kwa kampuni mbalimbali, Jayrutty iliibuka mshindi kutokana na ubora wa ofa yao.

“Jayrutty wameshinda zabuni hiyo kwa ajili ya kuuza na kusambaza bidhaa zote za Simba. Kila mwaka klabu itapokea Shilingi bilioni 5.6, kiasi ambacho kitaongezeka kwa asilimia 10 kila mwaka,” amesema Muba.

Mkurugenzi wa Jayrutty, Joseph Rwegasira, amefafanua kuwa mkataba huo hauishii tu kwenye bidhaa bali unajumuisha miradi mikubwa ya maendeleo. Moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki kati ya 10,000 hadi 12,000.

“Mbali na uwanja, tumeamua pia kuwapa basi la kisasa aina ya Irizar kwa ajili ya safari zao. Tutaongeza mchango wa Shilingi milioni 100 kila mwaka kwa ajili ya Simba Day, na tutaboresha chumba cha utabibu cha klabu,” amesema Rwegasira.

Aidha, Jayrutty itakuwa ikitoa Shilingi milioni 470 kila mwaka kwa ajili ya motisha kwa wachezaji wa Simba, ikiwa ni pamoja na posho kutokana na mafanikio kwenye mashindano mbalimbali.

Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa motisha hiyo pia itakuwa ikiongezwa kila msimu. Katika kuhakikisha Simba inajipambanua kimataifa, Jayrutty pia italeta jezi mpya zenye ubora wa kidunia.

“Niwahakikishie Wanasimba, msimu huu timu itakuwa ya tofauti sana. Jezi zitakuwa na ubora wa kimataifa, na klabu itazidi kupata heshima na thamani kubwa,” amesema.

Kupitia mkataba huu, Simba SC inaonekana kujiandaa kwa hatua kubwa zaidi kitaifa na kimataifa, ikiwa ni ishara kuwa klabu hiyo inalenga kuendelea kuwa kinara wa soka la Afrika Mashariki.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button