Nyumbani

Simba kuanza kazi upya

Malengo Yahamia Ligi Kuu na Fainali ya CAF

DAR ES SALAAM: BAADA  ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, uongozi wa klabu ya Simba haupotezi muda katika shangwe, sasa wanaelekeza macho yao katika majukumu mazito yaliyoko mbele, yakiwemo michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na maandalizi ya fainali ya CAF.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah maarufu kama Try Again, amesema uongozi umeamua kuweka kando furaha ya awali na kuingia kazini upya  kuhakikisha wanatimiza malengo yao msimu huu.

“Sisi viongozi tumeona bado muda wa kufurahi; hiyo ni kazi ya mashabiki kwa sasa. Tuna kazi kubwa mbele yetu, kujiandaa kwa mechi za Ligi Kuu na kupanga mikakati ya fainali ya CAF,” amesema Try Again.

Simba SC wamerejea nchini wakitokea Afrika Kusini walikofanikiwa kuitupa nje Stellenbosch FC kwa jumla ya mabao 1-0, na  kufuzu kucheza fainali ya CAF kwa mara ya pili  katika historia yao.

Timu hiyo sasa inajiandaa kuvaana na Mashujaa FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa Ijumaa, Mei 2, katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.

Try Again amesema  Simba inahitaji kuonesha uwezo wake katika kila mashindano, ikiwa ni pamoja na kuwania ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la FA,  hasa kutwaa Kombe la Shirikisho la CAF mbele ya mashabiki wao nyumbani.

“Simba haibebi jina lake tu, bali inapeperusha bendera ya Tanzania. Ni jukumu letu sote, Watanzania, kuhakikisha kombe hilo linabaki nyumbani katika mchezo wa fainali Mei 25, Uwanja wa Benjamin Mkapa,” aliongeza.

Amesema Kwa sasa, mashabiki wa Simba wanalo jambo moja tu la kufanya , kuiunga mkono timu yao katika hatua hizi za mwisho za mafanikio ya kihistoria.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button