BurudaniFilamu

Siku saba zilizoacha mshangao nchini Uganda

WATU wa kazi waliojipanga kisawasawa wanaiteka ndege aina ya Air France Flight 139 iliyo
safarini kutoka jiji la Tel Aviv nchini Israeli kuelekea jijini Paris, Ufaransa.

Ni watu wanne tu, magaidi walio tayari kwa lolote. Wawili Wapalestina na wawili Wajerumani wanaiteka ndege hiyo ya Ufaransa inapotaka kutua katika Kiwanja cha Ndege
cha Athens, Ugiriki, na kuwalazimisha marubani wa ndege hiyo kwenda kujaza mafuta nchini Libya kabla ya kuelekea Entebbe, Uganda.

Lengo la utekaji wao ni kuwatumia mateka wa Waisraeli takribani 84 kuibua majadiliano na serikali ya Israeli juu ya masuala yanayohusu watu wa Palestina. Wanaamini kwamba dikteta wa Uganda, Idi Amin Dada, ambaye msimamo wake kidini unaipinga Israeli,
atawaunga mkono.

Mmh… kazi ipo! Hawa jamaa wanaonekana kuwa ni watu wa kazi kweli kweli! Ni magaidi hatari ambao baada ya kuiteka ndege hiyo wanawashikilia abiria na wafanyakazi wa ndege hiyo katika Kiwanja cha Ndege cha Entebbe nchini Uganda.

Hawaishii kuwashikilia mateka tu bali wanadai fidia ya dola milioni 5 kwa ndege hiyo na kuachiwa kwa Wapalestina na wale wanaowaunga mkono wapiganaji wa Palestina 53, ambao 40 kati yao walikuwa wamefungwa katika magereza nchini Israeli.

Dah! Ni jambo zito kwelikweli kwa nchi ya Israeli, nchi ya watu wanaoamini kuwa wao ndio
‘mwanzo na mwisho’ lakini sasa wameshikwa sharubu. Hata hivyo, juhudi za kidiplomasia zinashindwa.

Sasa Serikali ya Israeli, ikiongozwa na Waziri Mkuu, Yitzhak Rabin, inaamua kuionesha dunia kuwa wao ndio alfa na omega. Kwanza wanaamua kukataa tena mpango wa majadiliano yoyote na watekaji hao.

Pili wanaanzisha misheni ya siri ya kuwaokoa mateka wa Kiyahudi bila kushiriki katika mazungumzo. Ni operesheni kabambe, ASLAY miaka 10 ya muziki na nyimbo 100 operesheni ya aina yake ya uokoaji inayopewa jina la ‘Operesheni Entebbe’.

Wanakitumia kikosi maalumu cha makomando wao, na kinachotokea baada ya hapo kinaiacha dunia mdomo wazi. Ni siku saba zinazoacha mshangao nchini Uganda!

Filamu ya 7 Days in Entebbe kama inavyojulikana nchini Marekani, ingawa sehemu nyingine inajulikana kama ‘Entebbe’, ni filamu ya aksheni ya dakika 107 iliyotoka mwaka 2018 nchini Marekani.

Imeandikwa na Gregory Burke na kuongozwa na José Padilha. Filamu hii inasimulia kuhusu operesheni maalumu ya uokoaji wa mateka wa Kiyahudi mwaka 1976, ambapo waigizaji mwanadada Rosamund Pike na Daniel Brühl wameonesha uwezo mkubwa kwa kucheza kama magaidi wa Kijerumani; Brigitte Kuhlmann na Wilfried Böse.

Zipo filamu kadhaa ambazo pia zinasimulia kuhusu operesheni Entebbe kama ‘Victory at Entebbe’, ambayo ilikuwa tamthilia ya runinga iliyotoka mwaka 1976 nchini Marekani; ‘Raid on Entebbe’ ya Marekani ya mwaka 1977; na ‘Operation Thunderbolt’ ya Israeli ya mwaka 1977.

Pia filamu kama ‘The Last King of Scotland’ iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa nchi za Uingereza na Ujerumani na kutoka mwaka 2006 imegusia tukio la uokoaji mwaka 1976.

Pia filamu ya ‘The Delta Force’ iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa nchi za Israeli na Marekani na kutoka mwaka 1986, kwa kiasi kikubwa wazo lake lilipatikana kutokana na tukio la Entebbe.

Hata hivyo, tofauti na filamu zilizotangulia kuhusiana na operesheni hii, filamu hii ya 7 Days in Entebbe inakiweka mapema kifo cha Yonatan ‘Yoni’ Netanyahu (kaka wa Waziri Mkuu wa
Israel, Benyamin Netanyahu), katika shambulio la kiwanja cha ndege. Yonatan Netanyahu
alikuwa mmoja wa makomandoo wa uokoaji.

Mwongozaji wa filamu ya 7 Days in Entebbe, Padilha, anasema kuwa kufanya hivyo kumetokana na mahojiano na pia washiriki waliokuwepo kwenye tukio hilo. Ingawa utayarishaji wa filamu hii uliongozwa na utafiti wa 2015 wa mwanahistoria wa Uingereza, Saul David wenye jina la ‘Operation Thunderbolt’.

Washiriki waliohojiwa ni pamoja na wafanyakazi wa ndege ya shirika hilo la Ufaransa waliokuwa pamoja na mateka wanaowasilishwa kwa njia ambayo inatofautiana na ushahidi mwingine uliokusanywa na mwanahistoria Saul David.

Lakini kama ilivyo kwenye filamu ya 7 Days in Entebbe, na kitabu cha Saul David, imewekwa wazi kuwa yapo makosa mengi yaliyofanyika na kidogo misheni ya uokoaji ishindwe kutokana na makosa ya Yonatan Netanyahu – hasa uamuzi wake wa kupiga risasi kwa walinzi wa Uganda wakati timu ya uokozi inakaribia jengo walimowekwa mateka.

Hata hivyo, kuna stori nyingine kuwa uokoaji ulifanikiwa sana, ulipangwa kwa umakini na ulifanywa kikamilifu na Yonatan kama kiongozi bora wa kikosi maalumu, na amekuwa
akichukuliwa kama shujaa na muongozaji katika operesheni hii.

Lakini ukweli, ndiye aliyetaka kusababisha operesheni ishindwe. Katika filamu hii, muongozaji aliamua kushughulikia usahihi wa kihistoria katika matukio kadhaa
yaliyotokea na kuyaweka ndani ya filamu hii.

Baada ya kutoka filamu hii ikakumbana na ukosoaji mkubwa japo inaonesha tukio muhimu katika uhusiano wa Israeli na Palestina, ambalo limekuwa la kihistoria. Filamu hii imetoka
rasmi Machi 16, 2018 nchini Marekani na baadaye nchini Uingereza mnamo Mei 11, 2018.

Hata hivyo, ilianza kuoneshwa katika Tamasha la 68 la Filamu la Kimataifa la Berlin mnamo Februari 19, 2018 na hadi sasa imefanikiwa kuingiza dola milioni 9.6 kwenye maonesho ya
filamu.

 

0685 666964 au bhiluka@ gmail.com

Related Articles

Back to top button