SHIMIWI watoa msaada kwa wahitaji Tanga

WACHEZAJI walioshiriki Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) wametoa msaada wenye thamani ya sh milioni 4.5 kwa makundi yenye uhitaji mkoani Tanga.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo wa chakula na mahitaji mengine katika vituo vya watoto yatima, wenye mahitaji maalum na wazee Katibu wa SHIMIWI Alex Temba amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona jamii hiyo ina uhitaji wa msaada.
Temba amesema kuwa watumishi ambao ni wanaSHIMIWI wameona ni vyema kurudisha furaha na kile ambacho serikali imewapa kwenye vituo mbalimbali kama fadhila kwao.
“Kipekee wanashimiwi wanamshukuru Rais Samia kwa kurudisha michezo hii na sisi tunamuahidi siku zote popote tutakapokwenda kipekee tutatenga siku maalumu kwa ajili ya kurudisha kile ambacho serikali imetupa kwa ajili ya watu wenye mahitaji mbalimbali, “amesema Temba.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo Mlezi wa kituo cha kulea watoto yatima cha nyumba ya furaha Irene Augustino ameshukuru kwa msaada huo na kusema kuwa umekuwa sehemu ya baraka kwa watoto hao.
Michezo hiyo ya 36 ya SHIMIWI ilifanyika kwenye viwanja vya Polisi Chumbageni, Bandari, TANROADS Mizani, shule ya sekondari Popatlal, Usagara na Galanos ikihusisha mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, riadha, karata, bao, drafti, kurusha tufe na kuendesha baiskeli.