Africa

Shime: Mechi dhidi ya Ethiopia haikuwa rahisi

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars, Bakari Shime, amesema licha ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake ‘WAFCON’ mechi hiyo haikuwa rahisi kama wengi walivyotarajia.

Akizungumza baada ya mchezo huo uliochezwa Dar es Salaam jana Shime alisema: “Nashukuru Mungu tumepata matokeo mazuri, lakini mechi haikuwa rahisi, ilikuwa ngumu,”

“Tulianza mchezo kwa kutumia mfumo wa mabeki watatu ili kuongeza nguvu katikati ya uwanja na pia kuwa na washambuliaji wawili juu. Lengo lilikuwa kufunga mabao mengi, lakini hatukufanikiwa,” aliongeza.

Shime alisema wapinzani walilazimisha Twiga Stars kucheza chini kutokana na presha yao kubwa, lakini katika kipindi cha pili walifanya mabadiliko yaliyoongeza kasi ya mchezo.

“Kipindi cha pili tulibadilika na tulicheza kwa kasi zaidi, ingawa hatukupata mabao mengi. Hata hivyo, tunashukuru kwa ushindi huu muhimu,” alisema.

Nahodha wa timu hiyo, Opa Clement, naye alikiri kuwa mchezo ulikuwa mgumu lakini muhimu kwao.

“Ulikuwa mchezo mgumu kwetu na muhimu. Tulitaka kupata matokeo mazuri nyumbani ili tukienda ugenini iwe rahisi kutafuta matokeo,” alisema Opa.

“Sasa tunarudi mazoezini kusikiliza maelekezo ya mwalimu kuelekea mchezo wa marudiano. Ushindi huu umetupa nguvu na morali zaidi, tukijua tumebakiza dakika 90 za mapambano ili kufuzu,” aliongeza.

Twiga Stars wanatarajia kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Ethiopia wiki ijayo mjini Addis Ababa.

Related Articles

Back to top button